Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tulia achafua ‘hali ya hewa’ Bungeni
Habari za Siasa

Tulia achafua ‘hali ya hewa’ Bungeni

Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Spread the love

KWA mara nyingine Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameingia katika mvutano na wabunge wa vyama vya upinzani baada ya kuzuia kujibiwa kwa baadhi ya maswali yaliyoulizwa Bungeni kwa madai kuwa maswali hayo si ya kisera, anaandika Mwandishi wetu.

Kitendo cha Dk. Tulia kuzuia kujibiwa kwa baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kilisababisha mvutano uliodumu kwa zaidi ya dakika 15, baada ya wabunge kutoafikiana na uamuzi huo.

Mbowe aliuliza maswali hayo katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu Bungeni, ambapo alitaka kujua ikiwa kuwafunga viongozi wakiwemo wabunge, madiwani na wanachama wa vyama vya upinzani ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali ya awamu ya tano.

“Je Mheshimiwa Waziri Mkuu, madamu rais ameshatangaza kuwa kusudio lake ni kufuta vya vya upinzani kabla ya mwaka 2020, haya yanayoendelea katika awamu ya tano ni sera au ni utekelezaji wa sera ya kuua upinzani ya serikali yako na mheshimiwa Magufuli?” alihoji Mbowe.

Hata hivyo Dk. Tulia alimzuia Majaliwa Kassim, Waziri Mkuu kujibu maswali kuhusu kufungwa kwa wabunge na madiwani wa Chadema kwa madai kuwa maswali hayo ni ya kisheria, huku akimtaka kujibu maswali ya kisera tu.

Akijibu maswali hayo Waziri Mkuu amesema, “Kwanza, nataka nikanushe kwamba rais hajawahi kutangaza kutaka kuvifuta vyama vya upinzani.

Pili, nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu na ipo Serikali, Mahakama na Bunge – hakuna muhimili unaoingilia mwingine na siwezi kuzungumzia mambo yaliyopo mahakamani.”

Ndipo Mbowe alipouliza swali la nyongeza, akitaka kujua iwapo Waziri Mkuu atakuwa tayari kujiuzulu iwapo ushahidi utatolewa na kuthibitisha kuwa Rais Magufuli amewahi kutoa kauli ya kukusudia kuua upinzani kabla ya mwaka 2020.

“Kauli ya kukusudia kuhakikisha mpaka 2020 hakuna upinzani ni kauli ya rais, na kwasababu hii ni kauli iliyotolewa na rais Je, tukileta ushahidi katika Bunge hili juu ya kauli yake ya kukusudia kutokuwepo kwa upinzani utakuwa tayari kuwajibika kwa kujiuzulu?” alihoji.

Hata hivyo Dk. Tulia alizuia swali hilo kwa madai kuwa suala la Waziri Mkuu kujiuzulu ni la kikatiba na si la kisera, hata hivyo wabunge mbalimbali waliwasha vipaza sauti na kusema, “Hilo ni swali la kisera!”

Dk. Tulia aliamua kumwita Mbunge mwingine ili aulize swali kwa Waziri Mkuu, hata hivyo wabunge wa upinzani walipinga kitendo hicho na kuibua zogo lililodumu kwa muda kabla ya naibu Spika kumuomba Mbowe awatulize wabunge hao.

“Mheshimiwa Mbowe, naomba uwambie watu wako watulie…hawa watu wako wa upande huu wanataka kusikiliza mawaz yako na si ya mtu mwingine…waambie watulie ili tuendelee na ratiba yetu..nakuruhusu uongee naye,” alisema Dk. Tulia huku wabunge wakimjibu “Hakuna watu wa Mbowe humu.”

Baadaye wabunge walitulia na kikao kuendelea mara baada ya Mbowe kuzungumza, ambapo alisisitiza kuwa maumivu ambayo wapinzani wanakumbana nayo ndani ya taifa lao kutoka kwa utawala wa awamu ya tano hayavumiliki.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi kuzikwa Machi 2 visiwani Unguja

Spread the loveMWILI wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania,...

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

Habari za Siasa

Babu Owino: Vijana msibaki nyuma

Spread the loveMbunge wa Embakasi Mashariki nchini Kenya, Paul Ongili Owino maarafu...

error: Content is protected !!