February 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tukio la kutekwa kwa MO Dewji laiibua LHRC

Spread the love

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani tukio la kupotea kwa Mfanyabiashara, Mohammed Dewji lililotokea jana alfajiri katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam, huku kikitoa wito kwa serikali na vyombo vya dola kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapatikana akiwa hai. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kupitia tamko lake lililotolewa leo tarehe 12 Oktoba 2018 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Felista Mauya, imeitaka serikali kuridhia mkataba wa kimataifa wa ulinzi dhidi ya mateso, ukatili, vitendo na adhabu zinazotweza utu wa mtu wa mwaka 1984 ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na usalama wa raia.

“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaikumbusha Serikali ya Tanzania kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi Dhidi ya Mateso , Ukatili , Vitendo na Adhabu Zinazotweza Utu wa Mtu wa mwaka 1984 kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na usalama wa raia.

Kituo pia kinalihamasisha jeshi la polisi kuchukua hatua stahiki kuhakikisha Mo Dewji anapatikana, watuhumiwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria sambamba na kuchukua hatua za madhubuti kukabiliana na vitendo vinavyotishia usalama wa raia na uvunjifu wa haki za binadamu kwa ujumla,” inaeleza sehemu ya tamko hilo.

Katika hatua nyingine, LHRC imesema imepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa za kutekwa kwa Mo Dewji, na kwamba inaungana na marafiki wa haki nchini na kote ulimwenguni kutuma salamu za pole kwa familia ya mfanyabiashara hao.

“Tukio la kutekwa kwa Mo Dewji ni mwendelezo wa matukio yanayotishia usalama wa raia na haki ya usalama binafsi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Bindamu Tanzania 2017 matukio takribani 38 ya watu kushambuliwa na kutekwa yaliripotiwa mwaka 2017. Katika baadhi ya matukio hayo wahanga waliripotiwa kuuawa, kujeruhiwa na wengine mpaka sasa taarifa zao hazijulikani.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinakemea vikali matukio haya yanayokiuka haki za binadamu pamoja na haki ya ulinzi binafsi. Haki hizi kwa ujumla zinatambuliwa na kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu ambao Tanzania imeridhia. Tunawasihi raia wema kuendelea kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mamlaka husika ili kuendelea kudumisha ulinzi wa haki za binadamu na usalama nchini Tanzania,” inaeleza sehemu ya tamko hilo.

error: Content is protected !!