Saturday , 2 December 2023
Home Kitengo Maisha Elimu Tuhuma za rushwa ya ngono vyuoni, pasua kichwa
ElimuHabari za SiasaTangulizi

Tuhuma za rushwa ya ngono vyuoni, pasua kichwa

Spread the love

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Faustine Bee, amewachongea baadhi ya wahadhiri wenzake katika chuo hicho kwa Rais John Pombe Magufuli. Anawatuhumu kujihusisha na vitendo vya ngono dhidi ya wanafunzi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea). 

Akizungumza mbele ya Rais Magufuli, katika mahafali ya 10 ya chuo hicho kikubwa nchini, Prof. Bee amesema, “baadhi ya wahadhiri wa UDOM wanatumia nafasi zao kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike.”

Kupatikana kwa taarifa hizi na hata kukiri kwa Makamu Mkuu wa UDOM kuwa ndani ya chuo chake kumesheheni vitendo vya ngono, kumekuja mwaka mmoja, tokea Dk. Vicensia Shule, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuibuka na kudai kwamba rushwa ya ngono imekithiri chuoni humo.

Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Dk. Shule alisema, “ndani ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, vitendo vya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wahadhiri dhidi ya wanafunzi, vinaonekana kama mambo ya kawaida.”

Dk. Shule alisema, alitaka kumueleza rais Magufuli jambo hilo, wakati alipofika kwenye chuo hicho, Novemba mwaka jana, lakini alishindwa kwa sababu ya kuwaogopa walinzi wake.

Rais Magufuli alizuru chuo hicho kwa lengo la kufungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa, iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwalimu. Julius K. Nyerere) jijini Dar es Salaam.

Aliandika: “Baba @MagufuliJP umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli.”

Ingawa hakueleza ni rushwa ya aina gani iliyokithiri, katika vyuo vikuu vingine kumekuwepo na tatizo la wahadhiri na wanafunzi kutumia ngono katika kutoa alama katika mitihani.

Aidha, baadhi ya wahadhiri hutuhumiwa kudai ngono kutoka kwa wenzao ndipo wawapandishe vyeo vyuoni.

Lakini kwa upande wa Prof. Bee yeye anasema, baadhi ya wahadhiri wa UDOM, wamekuwa wakitumia mamlaka yao kushinikiza kupewa ngono na wanafunzi wa kike, kwa lengo la kuwapa afueni katika mitihani yao.

Amesema, hata wanafunzi nao, hujilengesha kwa wahadhiri kwa ajili ya kuwapa ngono, ili wafaulishwe kwenye masomo yao.

Prof. Bee amesema, katika chuo chake hicho, kuna dosari za vitendo hivyo, na kwamba tayari uongozi umeunda kamati ya maadili kuchunguza na kudhibiti unyanyasaji wa kijinsia wa rushwa ya ngono kwa wanafunzi.

Amesema, kamati hiyo imeundwa na George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Wafanyakazi wamekuwa wakiomba rushwa ya ngono au fedha kwa wanafunzi ili kuwafaulisha. Wapo pia wanafunzi wanaowalazimisha wafanyakazi kuwapa rushwa ya ngono ili kufaulishwa masomo yao,” amesema Prof. Bee.

Hata hivyo, Prof. Bee amesema, unyanyasaji wa kingono haupo kwenye chuo hicho tu, tatizo hilo lipo kwenye maeneo mengine mengi; uongozi wa chuo hicho utamchukulia hatua kali yeyote anayejihusisha na tabia hiyo.

Katika hatua nyingine, Makamu Mkuu huyo wa UDOM amesema, chuo chake kilitarajia kudahili wanafunzi 15,000 kwa mwaka huu wa masomo. Lakini hadi kufikia jana, 21 Novemba, wameweza kudahili wanafunzi 9,674. Amesema, ni mtarajio ya uongozi wake, kuongeza idadi hiyo ya wadahiliwa kufikia wiki ijayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Elimu

Janeth Mbene apongeza HKMU, ataka wahitimu wajiajiri

Spread the loveWAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), ...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mwalimu jela miaka mitatu kwa rushwa

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi, wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu...

Habari za Siasa

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua programu ya...

Habari za Siasa

AG aiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia mawakili wanaokiuka maadili

Spread the loveMWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Eliezer Feleshi, ameagiza Kamati...

error: Content is protected !!