BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limewataka waumini wake kufanya toba ya kweli ili kubadili mioyo mibovu. Anaripoti Ragina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Katika ujumbe wake wa Kwaresma ya mwaka 2021, baraza hilo limeeleza, ubinafsi na uchoyo huathiri hata utendaji wa taasisi mbalimbali kiasi cha kusababisha watendaji kujifikiria wao zaidi ya ufanisi wa huduma walizokabidhiwa.
“Toba ndio msingi wa Kwaresima. Hata Jumatano ya Majivu tunakumbushwa hilo kwa kinywa cha nabii Yoel akisema,’Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote…’ (Yoel2:12). Kurarua mioyo ni kuingia ndani ili kujichunguza na kuruhusu moyo usikie sauti ya Mungu.”
“Matokeo yake ni kuongezeka kwa maskini na fukara katika jamii zetu. Kwa mfungo huu wa Kwaresima, tunaalikwa kufanya toba ambayo itatusaidia kubadilishalina misimamo yetu mibovu, kama vile dhuluma na uonevu kwa wanyonge,” umeeleza ujumbe huo.
Kwenye ujumbe huo, uliotolewa na Maaskofu 33, wenye kurasa 29 ukiwa na kichwa cha habari “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu…” (Zab 95:7-8) unawataka, waumini kuacha ubinafsi na uchoyo matokeo yake ni dhuluma na uonevu kwa wanyonge.
TEC imekumbusha waumini kutumia kipindi hiki cha mfungo wa Kwaresma, kuushinda ubinafsi na uchoyo.
“Mfungo huu wa Kwaresima utupatie fursa ya kuushinda ubinafsi na uchoyo ambavyo hufanya mioyo yetu kuwa migumu.
“Mambo haya mawili; ubinafsi na uchoyo, huathiri sana jamii yetu ya Kitanzania kiasi cha kubadili hata mifumo yetu ya maisha ya kindugu tuliyoizoea,” umeeleza ujumbe huo.
Na kwamba, katika jamii ya sasa, asilimia kubwa ya wenye nacho wamekuwa wachoyo, kwa kushindwa kutoa misaada kwa wahitaji.
“Mioyo migumu hufunga milango isione mahitaji ya jamii inayoizunguka. Katika jamii ya sasa, ni jambo la kawaida kuona wengine wana kila kitu cha kuendesha maisha, mfano chakula, mavazi na malazi; huku tukishuhudia kundi kubwa la wanajamii wakikosa chakula na malazi,” umeeleza ujumbe huo.
TEC limewaomba waumini kutumia kipindi hiki cha Kwaresma kilichoanza Jumatano ya 17 Februari 2021, kuomba toba kwa Mungu, ili mioyo ilainike kwa ajili ya kutenda yaliyo mema.
“Kurarua mioyo ni kuruhusu kubadilika lakini huku kurarua mioyo kunapaswa kuwa katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu, Kijamii, kiroho, kiuchumi na kisiasa,” umesema ujumbe huo.
Ujumbe huo wenye kurasa 29, uliobeba ujumbe kutoka Kitabu cha Zaburi 95:7-8 ‘Ingekuwa heri leo msikie sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu’ umewakumbusha Watanzania kurudi kwenye misingi ya Mungu katika kiroho, kijamii, uchumi na kisiasa.
“Ingekuwa heri msikie sauti yake leo,” nikauli iliyojikita kwenye ukaidi na utukutu wa wanaoambiwa. Waisraeli walitakiwa walegeze mioyo yao na waambilike; na ndivyo tunavyotakiwa kuwa na sisi.
“Wao walikuwa Israeli ya zamani, sisi ndiyo Israeli mpya. Wao walikuwa vizazi vya Ibrahimu moja kwa moja (Yn8:33-47), sisi ni kwa njia ya ubatizo wetu (rej.Rum 11:11-32, Efe 3:6), walioambiwa kwanza wamepita, kumbe sasa maneno hayo yanatuhusu mimi na wewe,” unaesema ujumbe huo.
Kuhusu uchumi, baraza hilo limeshauri waumini wake kubadili mioyo yao katika kusikia kilio cha wanyonge wanaoteseka kiuchumi.
“Kati ya matokeo tarajiwa ya Kwaresima ni kubadilika kwa mioyo yenu kuelekea mazingira mazuri ya kiuchumi yenye kujali watu wote.
“Utendaji mbaya umewafanya wachache kufaidi matunda ya kiuchumi na kuwaacha wengi wakiwa hawana fursa ya kujikwamua kiuchumi,” umeeleza waraka huo na kuongeza:
“Kwaresima hii inatualika kujiangalia ndani ya mioyo yetu kuona namna tunavyoweza kusikia kilio cha wanyonge wanaoteseka kiuchumi.”
Leave a comment