May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tucta: Mishahara haijaongezwa miaka nane, ianzie Sh. 970,000

Kaimu Katibu Mkuu TUCTA, Said Wamba

Spread the love

 

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aongese mishahara ya watumishi wa umma huku ikipendekeza kima cha chini kiwe Sh.970,000. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Jumamosi tarehe 1 Mei 2021, na Kaimu Katibu Mkuu TUCTA, Said Wamba, katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi), inayofanyikia kitaifa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Wamba amesema, mishahara ya watumishi wa umma na sekta binafsi haijapandishwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita mfululizo.

“Mishahara haijaongezwa kwa miaka nane kwa sekta binafsi na sita kwa watumishi wa umma, hali hii imesababisha kupunguza hali na mori wa kazi hivyo kupunguza ufanisi wa kazi na gharama za maisha zimeendelea kupanda.”

“Kima cha chini cha wafanyakazi zaidi ya miaka sita kimeendelea kuwa duni ukilinganisha na hali ya maisha,” amesema Wamba.

Amesema, kima cha chini kwa sasa kwa wafanyakazi wa majumbani ni Sh.40,000 hadi Sh.60,000 huku wa viwandani ikiwa ni Sh.100,000. Wakati kwa watumishi wa umma ni Sh. 300,000 ambazo zimetangazwa mwaka 2015.

Wamba amesema, Tucta ilifanya tatifiti mbili ikiwemo 2006 ambapo ulibaini kwamba kima cha chini cha mshshara kinachotosheleza ni Sh.315,000.

“2014 tulifanya utafiti na kubaini Sh.720,000 kwa wakati huo kingemuwezesha mfanyakazi kumudu kazi yake. Licha ya kutofikiwa kiwango hicho, mpaka sasa gharama za maisha zimeendelea kupanda na kuumiza watu wa sekta zote na kufanya wafanyakazi na familia kuishi chini ya mstari wa umasikini,” amesema Wamba.

Kaimu katibu Mkuu huyo amesema, shirikisho hilo linapendekeza kiwango cha chini cha mshahara kiwe Sh. 970,000 ambacho kinakidhi hali halisi ya maisha ya sasa.

error: Content is protected !!