September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TTCL yathibitisha ‘kufyeka’ wafanyakazi 550

Spread the love

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limethibitisha kutaka kupunguza wafanyakazi 550 kati ya 1,500 walioko nchi nzima, ambao hawana sifa za kitaalamu na kushindwa kuendana na kasi ya utendaji wa shirika hilo na serikali ya awamu ya tano. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na  TTCL hivi karibuni, inaeleza kuwa, zoezi la kupunguza wafanyakazi hao litatekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma kwa kuzingatia misingi ya haki, uwazi, utu na maridhiano.

“Jambo hili si geni ndani ya shirika kwa kuwa mchakato wake ulianza mwanzoni mwa 2017, kwa majadiliano yaliyoshirikisha wafanyakazi kupitia vyama vyao, mamlaka za serikali na wadau wengine wa TTCL ambao mara zote wamekuwa wakijulishwa kwa ufasaha juu ya maendeleo ya zoezi hili,” inaeleza sehemu ya taarifa ya TTCL.

Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa, TTCL inawasisitiza watumishi na wadau wote wa shirika hilo, kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao kama kawaida hadi pale taarifa nyingine zitakapotolewa.

Taarifa ya TTCL imekuja baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti mpango wake wa kupunguza wafanyakazi kufuatia kauli iliyonukuliwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Omari Nundu wakati akielezea hatua za TTCL katika kukabiliana na mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC).

Nundu aliieleza kamati hiyo ya bunge kuwa, idadi kubwa ya watumishi wa TTCL ni miongoni mwa sababu zinazochangia ukubwa wa gharama za uendeshaji wa shirika hilo.

error: Content is protected !!