January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TTCL yafilisika, yapata hasara ya bil 300, haikopesheki

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Airtel, Diego Gutierrez (kushoto) akiteta jambo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL, Kamugisha Kazaura

Spread the love

KAMPUNI  ya Simu Tanzania (TTCL), ambalo ni shirika kongwe la umma, sasa imefilisika kibiashara kutokana na ubia tata kati ya serikali na wawekezaji wenye mgongano wa kimaslahi katika sekta ya mawasiliano. Anaandika Deusdedit Kahangwa … (endelea).

Aidha, ubovu wa menejimenti, ubadhirifu wa fedha za umma, wafanyakazi waliokatishwa tamaa, ukosefu wa mtaji, madeni sugu, na mitambo iliyopitwa na wakati ndivyo vinavyochangia kuliua.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura, kampuni hii inachungulia kaburi kwa sababu imekuwa ikipata hasara mwaka hata mwaka kiasi cha kufikia hadhi ya “kutokopesheka.”

Dk. Kazaura ameiambia MwanahalisiOnline  kwamba kampuni ya TTCL imepata “hasara kubwa ya kiasi cha Sh. 335 bilioni mpaka kufikia mwaka 2013” jambo ambalo limeifanya “kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji hasi wa Sh. 88 bilioni.”

Kwa mujibu wa Dk. Kazaura, “kwa sasa Kampuni ya TTCL ni mufilisi,” hatua ambayo inatokana na “mbia mwenye hisa za asilimia 35, kutofanya uwekezaji mkubwa tangu aingie katika ubia na serikali mwaka 2001.”

Dk. Kazaura aliyasema hayo mjini Dodoma mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mawasiliano na Uchukuzi.

Nae Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, amesema mchakato wa kuondoka kwa Kampuni ya Airtel kutoka TTCL “uko katika hatua za mwisho.” Ameeleza kuwa tayari “makubaliano ya bei” ya hisa zinazodaiwa kumilikiwa na Airtel katika TTCL yamefikiwa “katika kikao cha majadiliano kilichofanyika tarehe 20 Novemba 2014.

Akielezea majadiliano yalivyokuwa, Profesa. Mbarawa  amesema  Kampuni ya Airtel iliafiki kuachia hisa inazomiliki ndani ya TTCL” na kisha Serikali kukubali “kuzinunua hisa hizo kwa Sh. bilioni 14.9” za Tanzania. 

Tayari “Baraza la Mawaziri liliidhinisha Serikali kununua hisa hizo” kwa mashrati kwamba malipo hayo yafanywe “baada ya taratibu za kisheria kukamilika” ili hatimaye “Serikali iweze kuimiliki TTCL kwa asilimia 100,” aliongeza Profesa Mbarawa.  

Profesa Mbarawa aliyatamka hayo wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, bungeni Dodoma hivi karibuni.

Kufuatia kuibuka kwa taarifa za malipo haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kupitia kwa msemaji wake wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, (CUF) Mohamed Habib Mnyaa, imehoji umakini wa serikali na kuitaka itekeleze mambo kadhaa.

· Kwanza, serikali imetakiwa kufafanua matakwa ya mkataba wa awali kati ya Serikali na Kampuni ya MSI na hatua za utekelezaji wa makubaliano ya mkataba huo mpaka sasa.

· Kueleza iwapo mkataba huo ulikuwa unairuhusu kampuni ya MSI kuuza hisa zake kwa makampuni mengine yaliyofuata kama vile Celtel, Zain na sasa Airtel.

· Kutoa ufafanuzi kuhusu uhalali wa maamuzi yake ya kuilipa kampuni ya Airtel Sh. 14 bilioni. 

Wadau wapinga malipo ya bilioni 14 kwa Airtel

Wakati mvutano huo ukiendelea kushika kasi wadau mbalimbali wamepinga hatua ya serikali kulipa mabilioni ya shilingi hayo kwa kampuni ya Airtel.

Kwa mfano, kati ya tarehe 16-18 Juni mwaka huu, wadau mbalimbali walikutana mjini Dodoma na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na mgogoro huu wa TTCL.

Pia, wadau kadhaa waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina walisema ni makosa kwa serikali kuilipa Airtel wakati haijawahi kuwekeza hata senti moja katika TTCL.

Kwa mfano, mdau mmoja ambaye ni mhandisi wa muda mrefu ndani ya TTCL, aliyejieleza kwa kirefu, lakini kwa masharti ya kutotajwa, akisema: 

“Ndani ya TTCL kuna tabaka la ngazi za mishahara ya watawala (TTCL1 hadi TTCL3), kwa upande mmoja, na tabaka la ngazi za mishahara ya makabwela (TTCL4 hadi TTCL10), kwa upande mwingine.

“Wafanyakazi wengi tulirundikwa katika tabaka la makabwela na tukapewa cheo cha ‘Team member’ lakini bila kuzingatia elimu, weledi, wala uzoefu wetu.

“Katika zoezi la mabadiliko hayo, Menejimenti iliongeza mishahara na kuboresha maslahi ya wafanyakazi wote walio katika tabaka la mishahara ya watawala lakini ikatutelekeza sisi wafanyakazi tulio katika tabaka la mishahara ya makabwela.

“Hata hivyo, sisi wafanyakazi wa ngazi za kawaida ambao hatukuboreshewa malipo ndio wazalishaji wakuu ndani ya TTCL.

“Kwa hiyo, sasa tunashangaa kuona kwamba sisi watu ambao tulisahaulika siku nyingi hatukumbukwi lakini wakati huo kampui ya Airtel ambayo haijawahi kuwekeza hata shilingi inatengewa mabilioni.

“Hivyo basi, kama serikali wanazo fedha za kichezea kiasi hicho waanza na maboresho ya maslahi ya wafanyakazi kabla ya jambo jingine lolote.”

Nae Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni chini ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia, Habib Mnyaa alipinga malipo hayo.

Amesema  kampuni ya Airtel hawapaswi kulipwa chochote kwa kuwa, mwekezaji huyu pamoja na watangulizi wake waliahidi kujenga “njia 800,100 za simu lakini wakashindwa, na badala yake hata njia 270,000 walizozikuta zimepungua kufikia njia 158,000 tu.”

“Kwa vile Airtel ilianzishwa kwa fedha, leseni na raslimali za TTCL, na mpaka sasa inatumia miundombinu ya TTCL kama vile jenereta, majengo, na viwanja, basi haipaswi kulipwa hata senti,” alisisitiza Mnyaa ambaye ni mbunge wa jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba.

Aliendelea, “Tukumbuke kwamba mwaka 1998 Kampuni ya Simu ilikuwa na mawasiliano ya simu katika makao makuu ya takribani wilaya zote nchini. Hivyo, tulitarajia kwamba kwa mwaka 2015 kampuni hii ingekuwa imefikisha mawasiliano hayo katika kila Kata ya Tanzania, lakini wapi. Huu ni udhalilishaji kwa Watanzania.”amesema.

Amesema  “Tofauti na Taarifa ya Wizara inavyopendekeza, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Hazina kusitisha makubaliano ya utoaji wa fedha hizo. Badala yake, turudi kwenye mkataba wa mwekezaji wa asili, MSI, ambaye amehamisha hisa zake kwa Bharti Airtel. Ufanyike uchunguzi kubainisha makubaliano katika mkataba na kuona kwa kiwango gani mwekezaji alitekeleza masharti ya mkataba.”

Mnyaa anamalizia kwa kusema tunapaswa “kuchunguza (MSI) alitakiwa kufanya nini, amefanya nini mpaka sasa, na kwa  hisa 35% alizopaswa kulipia alitoa fedha kiasi gani. Kama matakwa ya mkataba yametekelezwa ndio mambo mengine yaendelee. Vinginevyo Airtel alipwe dola moja tu na kufunga virago haraka.”

Ubovu wa Menejimenti ya TTCL

Kwa upande mwingine, tayari Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Asad, amemfikishia Rais Kikwete taarifa mbaya kuhusu TTCL.

Taarifa hizo zimemfikia Rais kupitia “Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014.”

Profesa Asad na ujumbe wake walikutana na Rais Kikwete 26 Machi 2015 Ikulu na kukabidhi ripoti hiyo. 

Ripoti inabainisha mambo kadhaa yanayoashiria ulegevu wa Menejimenti ya TTCL kama yalivyogunduliwa na CAG.

Kwanza, ilibainika Menejimenti ya TTCL imeshindwa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani ili kukabiliana na vihatarishi vya usalama wa kampuni.

Pili, Menejimenti imeshindwa kusimamia ipasavyo mfumo wa mishahara jambo ambalo lilitoa mwanya kwa mtumishi mmoja kutumia mfumo huo kuiibia kampuni kwa kujizidishia mshahara wake kwa kiasi cha Sh. 72 milioni.

Tatu, Menejimenti imefanya manunuzi ya bajaji 30 zenye thamani ya Sh. 156 milioni bila ya kuzingatia vyema Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2004. Hapa, Bodi ya Zabuni ya TTCL ilitumia utaratibu wa zabuni zuifu (restricted tendering) kinyume na maamuzi yaliyofanywa na Bodi ya Wakurugenzi walioidhinisha mchakato wa manunuzi wa ushindani wa kimataifa.

Nne, Menejimenti imefanya manunuzi ya magari 10 yenye thamani ya Sh. 1.25 bilioni pasipo kuzingatia vyema Sheria ya Ununuzi wa Umma. Kamati ya Tathimini ya Zabuni ilipendekeza zabuni hiyo itolewe kwa Toyota Tanzania pamoja na kwamba mzabuni huyu hakukidhi vigezo vingi vilivyoainishwa katika zabuni hiyo.

Tano, Menejimenti imeshindwa kudhibiti matumizi ya mafuta ya magari jambo ambalo liliingizia kampuni hasara ya Sh. 73.7.

Sita, Menejimenti imeruhusu manunuzi ya kiasi cha Sh. 45.7 bilioni nje ya mpango wa ununuzi wa mwaka. Hatua hii ni kinyume na matakwa ya kif. 45 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004 na Kanuni ya 25(3) ya Kanuni za Sheria ya Ununuzi ya Umma ya Tangazo la Serikali Na.97 la mwaka 2005. Kanuni hii inazitaka taasisi za umma kuandaa mpango wa ununuzi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo ndani ya mpango mkakati.

Saba, Menejimenti imefanya manunuzi yenye thamani ya Sh. 3.442 bilioni pasina kuzingatia viwango vya ukomo vilivyoainishwa kwenye jedwali la pili la Kanuni za Sheria ya Ununuzi Tangazo la Serikali Na.97 na 98 la mwaka 2005. Kiwango kilichozidishwa ni Sh. 1.742 bilioni.

Ukiukwaji wa matakwa haya ya kisheria unapaswa kupata idhini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi (PPRA) kama inavyoelekezwa na kifungu cha 31(3) cha Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2004. Lakini hakuna kibali kilichoombwa wala kutolewa na PPRA kwa ajili hiyo.

Kutokana na kasoro hizo, Mdhibiti na Mkaguzi ametoa mapendekezo makuu matatu:-

Kwanza, Menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ifikirie “kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote ambao ripoti hii imeainisha kuwa wamehusika katika kuisababishia kampuni hasara ya upotevu wa fedha.” 

Pili, “Wakurugenzi wa Bodi ya TTCL watoe mwongozo wa uadilifu na kutekeleza sheria za kukomesha udanganyifu.” 

Tatu,  “TTCL ihakikishe inafanya ukaguzi endelevu na usimamizi mzuri wa miamala inayofanyika katika mfumo wa hesabu wa Sunsystem, ili kudhibiti wizi kama uliofanyika kwenye mfumo wa uandaaji wa Mishahara.”

Ubia wenye utata kati ya serikali na wawekezaji

Taarifa kwamba kampuni ya TTCL sasa inashikilia mkia wa kibisahara katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania kutokana na serikali kuwakaribisha wawekezaji wenye mgongano wa kimaslahi katika sekta hii zinayo historia ndefu sasa.

TTCL ilianzishwa kwa mujibu wa sheria Na.20 ya 1993 na kupata leseni ya kuendesha biashara ya mawasiliano ya simu za mezani. Mwaka 1999 tayari TTCL ilikuwa imefanikiwa kutafuta leseni ya kuendesha biashara ya simu za mkononi pia kupitia kampuni tanzu iliyoiita Celnet Tanzania Limited.

Ofisi za Celnet Tanzania Limited zilikuwa Kijitonyama, Dar es Salaam, mkabala na jengo la Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC).

Uanzishwaji wa Celnet Tanzania Limited ilikuwa ni moja ya mbinu za menejimenti kujiimarisha kibiashara ndani ya ushindani zikiwepo kampuni mbili tu – Tigo na Tritel. Kumbukumbu zinaonesha mtaji wa Celnet Tanzania Limited ulikuwa ni Sh. 500 milioni.

Katikati ya harakati hizo, 21 Februari 2001, serikali iliamua kuibinafsisha TTCL kwa kuuza sehemu ya hisa. Serikali iliuza 35 kwa Dola 120 milioni kwa kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi.

Hata hivyo, kampuni ya MSI ililipa dola 60 milioni tu (nusu ya kiwango halisi) kwa madai kuwa wangelipa kiasi kilichobaki baada ya mahesabu kukaguliwa upya na mkaguzi huru. Hivyo, malipo waliyoyafanya yalikuwa ni sawa na bei ya hisa asilimia 17.5 pekee. Serikali ilikabidhi menejimenti ya TTCL kwa MSI pamoja na kasoro hiyo ya kutekeleza mkataba.

Baada tu ya MSI kushika mamlaka ya TTCL, ilibadilisha leseni na jina la kampuni ya Celnet Tanzania Limited kuwa Celtel Tanzania Limited, ambayo Novemba 2001 ilipewa leseni ya kuendesha simu za mkononi.

Kampuni ya TTCL ilipewa asilimia 40 ya hisa za Celtel Tanzania Limited, ambazo baadaye zilihamishwa na Serikali na kupelekwa Hazina. Profesa Mark Mwandosya alikuwa ni Waziri mwenye dhamana na TTCL wakati huo, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa Andrew Chenge.

Nyaraka mbalimbali zinaonesha kwamba MSI hawakuwekeza hata senti moja katika kampuni ya Celtel Tanzania Limited. Kinachoonekana ni kwamba, kabla ya kampuni ya MSI kuondoka TTCL mwaka 2005, walikuwa wamelipa ziada ya dola za Kimarekani 8 kati ya dola za Kimarekani 55 walizopaswa kulipa kama sehemu ya pili ya malipo ya hisa walizonunua katika TTCL.

Kwa ufupi, tangu kubinafsishwa kwa TTCL mwaka 2001, hisa zake zipatazo 35% zimekuwa zikiuzwa kwa mkopo kupitia utaratibu wa “mpokezano” kwa makampuni tofauti, yote yakiwa yanajitambulisha kama “wawekezaji” katika TTCL.

Mpokezano huo ni kama ifuatavyo: kutoka MSI kwenda Celtel International (2005), kutoka Celtel International kwenda Zain ya Kuwait (2008) na kutoka Zain ya Kuwait kwenda Bharti Airtel ya India (2010). Kampuni ya Bharti Airtel Ltd ya India ndio mmiliki wa Airtel Tanzania Ltd kwa sasa. Kumbukumbu zinaonesha kuwa wawekezaji hawa wote hawajawahi kuwekeza fedha yoyote ili kuimarisha TTCL.

Utafiti zaidi unaonesha MSI, Celtel International, Zain ya Kuwait na Bharti Airtel ya India wamekuwa “wawekezaji” na wakati huohuo “washindani” wa TTCL kibiashara katika sekta ya mawasiliano.

Kwa hivyo, haya ni makampuni yaliyokuwa na mgongano wa maslahi. Kwa sababu hii, wachunguzi wa mambo wanasema mgongano huu wa kimaslahi uliwasukuma “wawekezaji” hawa “kuihujumu TTCL kisayansi.”

Kwa mfano, utafiti wa Mwanahalisionline ndani ya TTCL umebaini kuwa mpaka leo hii, bado kampuni hii inatumia teknolojia ya mawasiliano duni kuliko teknolojia inayotumiwa na makampuni mengine ya mawasiliano hapa nchini.

Wakati Tigo, Airtel na Vodacom wamekuwa wanatumia teknolojia ya kisasa ya “Global System for Mobile Communication” (GSM), TTCL wamekuwa wanatumia teknolojia kongwe ya “Code Division Multiple Access” (CDMA).

Simu zinazotumia “simukadi” za teknolojia ya CDMA haziwezi kupokea “simukadi” za teknolojia ya GSM. Hivyo, wateja wenye “simukadi” za mitandao ya Tigo, Vodacom na Airtel hawaoni sababu ya kununua “simukadi” za mtandao wa TTCL kwani “simukadi” hizi hazingiliani na simu za mikononi zinazotumiwa na wateja hawa wa mitandao ya Tigo, Vodacom na Airtel.

Lakini, kama TTCL wangetumia teknolojia ya GSM kwa muda wote huo, wangekuwa katika nafasi nzuri ya kushindana wakiwa na nguvu katika soko la biashara ya simu za mkononi nchini.

Hivyo, ni wazi kwamba kikwazo hiki cha kitekinolojia kimechangia kuidhoofisha kiuwezo TTCL na hivyo kubaki ikichechemea.

Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) zinathibitisha jambo hili. Mpaka Desemba 2012 Tanzania ilikuwa na watumiaji wa simu za meani na mkononi wapatao 28,024,611.

Wateja hawa waligawanyika kama ifuatavyo: Vodacom (44%), Airtel (27%), Tigo (20%), Zantel (8.4), TTCL (0.82%), Sasatel (0.18%) na Benson (0.0037%).

Mhandisi mmoja ndani ya TTCL, aliliambia Mwanahalisionline  kwamba takwimu hizi ni ushahidi tosha kuonyesha kwamba “wawekezaji katika TTCL wameihujumu kampuni hii kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi uliogubika dhamira na maamuzi yao.”

Hoja hii inaimarishwa na ukweli kwamba jitihada za TTCL kuingia katika soko la mawasiliano ya simu za mkononi zinazotumia teknolojia ya GSM mpaka sasa limekwama.

Historia inajieleza vizuri: Muda mfupi baada ya TTCL kupata hisa katika kampuni ya Celtlel Tanzania Ltd, ilinyang’anywa hisa zote na zikahamishiwa HAZINA mara moja, kwa sababu ya madai kwamba, kwa mujibu wa leseni yake, TTCL haikuruhusiwa kuanzisha biashara ya simu za mkononi.

Hata hivyo, baadaye mwaka 2005, serikali iliondoa masharti hayo ya leseni dhidi ya TTCL. Lakini Celtel international, ambaye tayari alikuwa ni mwanahisa katika TTCL na hivyo mbia wa serikali, alipinga wazo la TTCL kujiingiza kwenye biashara ya simu za mkononi. Sababu ni moja tu hapa: alikuwa ni mshindani wa TTCL katika biashara hiyo.

Baada ya kuona hivyo, wafanyakazi wazalendo ndani ya TTCL waliamua kuingiza biashara hiyo kwa siri kupitia teknolojia ya “CDMA” maarufu kama “TTCL Mobile.” Kwa namna fulani, wazalendo waliidanganya Bodi ya TTCL kuwa teknolojia ya “CDMA” ilikuwa ni kwa ajili ya “Fixed Wireless” au “Wireless Local Loop (WLL).”

Lakini, ukweli, kwa siri walikuwa wamebuni “Full Mobile Solution” ili kujitanua kibiashara. Bodi ya TTCL iliruhusu biashara hii kwa kuwa haikufahamu ukweli wote. Hata hivyo baadaye Bodi ilipogundua iliamua kuzuia uwekezaji zaidi katika mradi huo. Kwa hivyo, mradi wa “TTCL mobile” ukashindwa kufanyakazi kama lilivyokuwa lengo wakati wa kubuniwa.

Leo, miaka 15 baada ya TTCL kubinafsishwa, bado kampuni hii inashika mkia katika biashara ya mawasiliano ya simu.

error: Content is protected !!