May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Treni yapata ajali Tanga, mmoja afariki watano wajeruhiwa

Spread the love

 

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema treni ya abiria yenye injini namba 9022 imepata ajali muda wa saa 10 alfajiri kati ya Mkalamo na Mvave wilaya ya Pangani mkoani Tanga leo tarehe 16 Januari, 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano (TRC), Jamila Mbarouk,  treni hiyo iliondoka Arusha muda wa saa 8:30 mchana siku ya Jumamosi kuelekea Dar es Salaam ikiwa na behewa 14 zilizobeba abiria 700.

Taarifa hiyo imesema, treni hiyo ilipofika eneo lililopo kati ya Mkalamo na Mvave (km 88) behewa tano zilipinduka na nyingine nne kuacha njia na kusababisha majeruhi watano.

Imesema katika majeruhi hao, wanaume ni watatu na wanawake ni wawili wakati kifo ni cha mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Hassan Lugano mwenye umri wa miaka saba.

“Behewa zilizopinduka ni namba 3614, 3527, 3605, 3526 na 3530 na zilizoacha njia ni behewa namba 3662, 3666, 4536 pamoja na behewa la huduma ya chakula na vinywaji.

“Majeruhi tayari wamepelekwa katika Zahanati ya Mkalamo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na wanaendelea vizuri,” imesema taarifa hiyo.

Shirika linaendelea na taratibu nyingine kurejesha huduma za usafiri pia linaendelea kufuatilia kwa karibu kufahamu chanzo cha ajali ili kuchukua hatua.

Aidha, shirika linatoa pole kwa familia ya marehemu na linawaomnbea majeruhi wa ajali wapate nafuumapema ili waweze kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa.

error: Content is protected !!