November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TRC yazungumzia gharama ujenzi reli ya kisasa

Spread the love

 

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limesema gharama inayotumika kujenga reli ya kisasa (SGR), ni ndogo ikilinganishwa na za nchi nyingine. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 28 Desemba 2021 na Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa, akitoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizodai kuwa gharama inayotumika katika ujenzi huo ni kubwa.

Ni katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa SGR, awamu ya tatu kipande cha Makutupora hadi Tabora, iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam.

“Pengine ningependa kutoa ufafanuzi, sababu sisi watendaji tunakuwaga hatuna nafasi ya kuzungumza tunapoona mengine yanazunguzmwa kwenye mtandao, kutokana na aidha maadili lakini muda unakuwa hauna. Mtendaji ni mtendaji, unakuwa muda wa kujibishana na watu hauna,” amesema Kadogosa.

Mkurugenzi huyo wa TRC, amesema gharama ya ujenzi wa reli hiyo kwa kilomita moja ni Dola za Marekani 3.997 milioni ikijumlishwa na kodi, bila kodi ni dola 3.387 milioni, kiwango kinachoendana na bei ya dunia.

“Nitoe maana ya gharama ya ujenzi tunaoufanya sasa, kwa maana ya gharama kwa kilomita kwa Tanzania, ukijumlisha na kodi ni dola 3.997 milioni. Na ni rahisi tu, chukua kilomita za roti zote nne halafu gawanya kilomita tunazojenga, ni kitu ambacho sio siri ni cha public kinapatikana,” amesema Kadogosa.

Kadogosa amesema, kiasi hicho cha fedha ni pungufu ya asilimia 50, ukilinganisha na gharama zinazotumika kujenga reli hiyo katika nchi kadhaa.

“Tulipoanza ujenzi huu tuliomba wizara kutupeleka kwenye nchi tisa ambazo zinajenga, au zinaendelea kujenga. Nisingependa kuitaja nchi, average (wastani) tuliyoikuta huko ya chini ilikuwa dola 5.6 milioni kwa kilomita moja , lakini kuna nchi nyingine zilikuwa zinaenda mpaka dola 6.2 milioni,” amesema Kadogosa.

Kadogosa amesema “maana yake ukiangalia katika ujenzi tunaoufanya ni makadirio ya asilimia 50 ya gharama za wengine , Rais mtu anapokuja kuandika kuna gharama ziko kubwa, ningependa kuweka rekodi vizuri, sababu uongo ukirudiwa unaonekana kama una ukweli kwa kiasi fulani.”

Aidha, Kadogosa amesema hadi sasa Serikali imewekeza Sh. 14.73 trilioni, katika mradi wa ujenzi wa SGR, ambapo kipande cha kwanza chenye urefu wa kilomita 300, kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, kimegharimu Sh. 2.7 trilioni.

Kipande cha pili kutoka Morogoro kwenda Makutupora mkoani Singida (Km 422), kimegharimu Sh. 4.4 trilioni, huku cha tatu kutoka Tabora hadi Isaka Mwanza (Km 341), kikigharimu Sh. 3.05 trilioni.

error: Content is protected !!