August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TRA yanasa wafanyabiashara 300

Spread the love

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata wafanyabiashara 300 kwa makosa ya kutotoa stakabadhi ama kuandika stakabadhi zenye bei ya chini tofauti na bei halisi ya bidhaa pia kutotumia mashine za kielektroniki (EFD), anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Alphayo Kidata, Kamishna Mkuu wa TRA amesema mamlaka hiyo haitowavumilia wafanyabiashara wanaoikosesha serikali mapato kwa kukwepa kulipa kodi kwa makusudi.

“Mwezi Aprili mwaka 2016 TRA imefanikiwa kukusanya Sh. 1.035 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 99.5 ya lengo la serikali la kukusanya 1.040 trilioni kwa mwezi huo, mafanikio haya yametokana na usimamizi mzuri katika ukusanyaji kodi pamoja na kuwadhibiti wakwepa kodi,” amesema Kidata.

Amesema kuwa, miezi 10 iliyopita TRA imefanikiwa kukusanya kodi kwa asilimia 99 kuanzia mwezi Julai 2015 hadi Aprili mwaka huu.

“Miezi kumi iliyopita TRA ilikusanya Sh. 11.092 ambayo ni sawa na asilimia 99 ya lengo letu tulilolenga kukusanya Sh. 11.20 trilioni kwa kipindi cha mwaka mzima,” amesema.

Aidha, Kidata amesema TRA inakusudia kwa kipindi cha miezi miwili iliyobaki yaani mwezi Mei na Juni kukusanya Sh. 1.4 trilioni ili kufikia ama kuvuka lengo lake kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016 la kukusanya Sh. 12.3 trilioni.

error: Content is protected !!