MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewapa Makatibu Wakuu 25 wa wizara mashine za kielektroniki (EFDs) 130 kwa ajili ya taasisi na mamlaka zenye wajibu wa kukusanya mapato ya serikali, anaandika Regina Mkonde.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Alphayo Kidata, Kamishna Mkuu wa TRA amesema kuwa, lengo la utolewaji wa mashine hizo ni kuhakikisha mamlaka inafikia na kuvuka lengo la kukusanya kodi Sh. 15.5 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
“Katika jitihada za kuhakikisha taasisi za serikali zinatumia mashine za kielektroniki kutoa risiti, TRA leo inatoa mashine hizi kwa ajili ya taasisi na mamlaka zenye wajibu wa kukusanya mapato ya serikali,” amesema.
Ameeleza kuwa, kila Katibu Mkuu atagawiwa mashine tano za EFDs zitakazosaidia kuhakikisha serikali inapata mapato yake na kwamba itaokoa mapato ya serikali ambayo yanapotea.
“Tunatarajia mashine hizi zitatumika mahsusi kutolea risiti na hivyo watumishi wote wa serikali ambao wanafanya marejesho ya matumizi mbalimbali wanatakiwa kuambatanisha risiti za mashine za EFDs,” amesema na kuongeza;
“Sambamba na hili, TRA bado inaendelea kudhibiti wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine za kielektroniki kwa kuwakamata na kuwatoza faini au kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria ili kuhakikisha inafikia na kuvuka lengo la kukusanya Sh. trilioni 15.5 kwa mwaka huu wa fedha,” amesema.
More Stories
Mapadri 25, Masista 60 waaga dunia Tanzania
TCRA yajitosa bei za vifurushi
Huawei yaunga mkono malengo endelevu UN