July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TRA kuandaa mpango mpya ukusanyaji kodi

Spread the love

WIZARA ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imeandaa mpango maalum wa ukusanyaji mapato wakilenga kuwafikia walipa kodi wote, anaandika Regina Mkonde.

Akipokea msaada wa Sh. 48 Mil kutoka Serikali ya Norway leo jijini Dar es Salaam Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha  amesema, serikali itahakikisha inakusanya kodi ili kuondoka katika utegemezi.

“Fedha tulizokabidhiwa na Serikali ya Norway tutazitumia kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi, kubuni mbinu za ukaguzi wa mahesabu hususan katika sekta mpya ya mafuta na gesi pamoja na kukiboresha kitengo cha kimataifa cha ukaguzi,” amesema Dk. Kijaji.

Amesema kuwa, serikali ikifanikiwa kusimamia ukusanyaji wa mapato haitashindwa kukusanya kiasi cha Sh. 22 Trilioni kwa mwaka ambayo ni sawa na bajeti ya nchi kwa mwaka mzima.

“Bajeti ya serikali ni trilioni 22 kwa mwaka, kama mapato yakikusanywa na kusimamiwa vizuri tunauwezo wa kukusanya trilioni 22 kwa mwaka na kuondokana na hali ya kuomba misaada kutoka kwa nchi rafiki,” amesema.

Dk. Kijaji amesema Serikali ya Norway imeridhishwa na utendaji kazi wa TRA pamoja na Wizara ya Fedha hali iliyochangia kuongeza fedha za msaada kwa mwaka wa 2016 ukilinganisha na mwaka 2015.

“Mwaka 2015 Norway ilitoa msaada wa Dola za Marekani milioni 3, baada ya kuona matumizi yake yamekwenda vizuri mwaka huu wametoa dola za kimarekani milioni 5 ambayo sawa na milioni 48,” amesema.

Tone Skogen, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Kifalme ya Norway amesema, serikali yake itaendelea kutoa msaada hasa katika sekta za mafuta na gesi pamoja na kilimo ambapo Norway ni muwekezaji mkuu wa sekta hizo.

“Serikali ya Norway imejikita katika sekta ya mafuta, gesi na kilimo ndiyo maana wawekezaji wa Norway utawakuta wamewekeza kwa asilimia kubwa kwenye maeneo hayo nchini Tanzania,” amesema Skogen.

Skogen amesema kwa muda mrefu Serikali yake imeshiriki kuijenga nchi kwa muda mrefu, na kwamba Naibu Waziri wa nchi hiyo ametoa mchango huo ili kuongeza jitihada na tija katika ukusanyaji kodi.

 

error: Content is protected !!