January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TPSF, JWT waungana kuleta mapinduzi

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk. Regnald Mengi (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja.

Spread the love

TAASISI ya Sekta Binafsi (TPSF), imeungana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) ili kuleta mapinduzi ya kibiashara, pamoja na kulinda uchumi nchini. Anaandika Sarafina Lidwino …(endelea).

Muungano huo pia, umeitaka Serikali kuwapigania na kuwapa maeneo ya kuwekeza na kuijenga nchi kiuchumi kuliko kuwapendelea Wachina wanaokuja kwa kasi kuwekeza nchini.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Regnald Mengi, amesema kuwa, wameamua kuungana kuwa na sauti moja kwa vile matatizo yao na changamoto zao zinaendana.

Mengi amesema, kuungana kwao pia kutazisaidia sekta zisizo rasmi kuingia katika sekta rasmi na kuweza kupata mawazo ya pamoja ili kuishauri serikali namna ya kuendeleza uchumi nchini.

“Pia, muungano huu tunaimani utaleta mabadiliko makubwa sana nchini kwetu, hususani vitendo vya rushwa ambavyo ni adui mkubwa sana wa maendeleo ya Watanzania. Rushwa ni mzigo mkubwa sana na maskini ndio wanaubeba mzigo huo,” amesema Mengi.

Mkutano huo umejumuisha viongozi mbalimbali wa JWT na TPSF, ambapo kila mmoja amekubaliana na muungano huo na kutoa mapendekezo mbalimbali.

Naye mwenyekiti wa JWT, Johnson Minja amesema, serikali inaruhusu kuongezeka kwa sekta zisizo rasmi kuliko zilizo rasmi, hivyo kuwanyima uhuru wafanya biashara wazawa.

Minja ameongelea kuhusu mpango wa serikali wa kuwapatia Wachina eneo la biashara la mradi wa Kurasini, akisema “hakuna mtu mwekezaji wakigeni anaweza kuleta maendeleo nchini kwa vile hawana uchungu kama wazawa.”

Kwa mujibu wa Minja, mradi huo wa Kurasini, ni mpanga wa serikali ambapo wanaamini kwa kuwapa maeneo Wachina ili kujenga soko, itawasaidia wananchi na kuongeza kipato kwa serikali, jambo alilodai sio kweli.

“Kwa mtazamo wa haraka, nchi hii sio huru kwani bado uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unategemea watu wa nje, kitu ambacho kinazidi kutukandamiza wafanyabiasha ndani ya nchi yetu,”amesema Minja.

error: Content is protected !!