
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Johson Minja (kulia) akijadiliana jambo na Makamu mwenyekiti wake, Mchungaji Silver Kyondo
TAASISI ya Sekta binafsi (TPSF), Umoja wa wafanyabiashara Tanzania (JWT), wameitaka serikali kusitisha mara moja mradi wa soko la wachina eneo la Kurasini Jijini Dar es Salaam unaoendelea. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).
Wameonya, Serikali isipokuwa sikivu na yenye kuelewa inaweza kusababisha machafuko kama yaliyotokea nchi jirani ya Afrika kusini, ambamo yalitokea kwaajili ya kutetea uchumi wao.
Wafanya biashara hao wamekutana leo Jijini Dar es Salaam, ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya kiuchumi pamoja na changamoto zinazowakabili.
Aidha, walikuwepo viongozi mbalimbali kutoka mikoa tofauti nchini, ambapo lengo kuu ni kukutana na viongozi wa TPSF ili kujadili masuala kama vile uwekezaji wa kigeni, uwezeshwaji wa wafanya biashara ndogondogo pamoja na mbinu za kukuza mitaji yao ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa ustawi wan chi na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa JWT Johnson Minja amesema, Serikali inatakiwa kuwajali wafanya biashara wa ndani kuliko kuwajali zaidi wawekezaji kutoka nje ambao wasiona na uchungu na nchi yetu.
Minja amesema, “hatuko tayari kuona tunatawaliwa ndani ya nchi yetu.serikali inatakiwa kutuongoza na kutuunga mkono kwani nguvu na pesa ya kuendesha miradi ya uchumi tunayo”amesema Minja.
Hata hivyo, wachangiaji mbalimbali ndani ya mkutano huo wamesema, wanaitaka serikali ichukue hatua kama walivyofanya nchi ya China kwa kuzuia wawekezaji wan je kuwekeza katika nchi zao.
Nae Katibu mkuu JWT, Mchungaji Kihondo amesema,serikali isipowasikiliza wafanya biashara wa ndani na kuendelea kuwathamini wachina ambao wanajengewa soko, “sisi tutachukua hatua na tutajibu kwa vitendo na kama serikali imepewa rushwa basi irudishe sisi tutawatimua na tutabaki na soko letu”
Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi amesema, watanzania wanatakiwa kuzitambua haki zao pamoja na kupata fursa zao ndipo wapewe wawekezaji.
Dk.Mengi amesema,Serikali inatakiwa kujua kuwa, hakuna mwekezaji wan je ambae anaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi ndani ya nchi yetu zaidi ya wazawa Tanzania ni ya watanzania sio ya watu wengine.
Amesema, “serikali itupe sisi hilo soko wanalotaka kupewa wachina halafu ione kama tutashindwa kuendesha uchumi wa nchi yetu.Sijawahi kuona serikali ya namna hii ambayo inawashibisha wageni kuliko wenyeji,” ameongeza Dk. Mengi.
Dk. Mengi aliwashauri wafanya biashara wadogowadogo kwamba, wanatakiwa kuona mbali kibiashara na wasikubali mtu kuwadharau na kuwakatisha tamaa .
Aidha, aliwataka kuwa na mawazo makubwa kabla ya kuanza kufanya biashara ili kusonga mbele, ili serikali isitafute sababu ya kuwawekea vipingamizi kumiliki masoko makubwa.
More Stories
Mapadri 25, Masista 60 waaga dunia Tanzania
TCRA yajitosa bei za vifurushi
Huawei yaunga mkono malengo endelevu UN