July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TP Mazembe mabingwa Afrika, Samata atwaa kiatu cha dhahabu

Spread the love

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefunga bao moja na kuseti moja, TP Mazembe ikitimiza dhamira ya kutwaa ubingwa wa Afrika baada ya kuifunga 2-0 USM Alger ya Algeria.

Mchezo huo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa uliofanyika Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, wenyeji walipata mabao yote kipindi cha pili.

Na Mazembe inatwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa jumla wa 4-1, baada ya awali kushinda 2-1 mjini Algiers Jumapili iliyopita.

Samatta leo aliwekewa ulinzi mkali na wachezaji wa USM hadi akalazimika kusubiri kufunga bao lake la saba katika michuano ya mwaka huu kwa penalti dakika ya 75, baada ya Rogger Asale kuangushwa.
Samatta naye akamsetia pasi nzuri Assale kufunga bao la pili katika dakika za majeruhi baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo.

Matokeo hayo yanamfanya Samatta pia awe mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu huu, baada ya kufikisha mabao saba, sawa na Bakri Al-Madina wa El-Merreikh ya Sudan.

Hii maana yake huu unakuwa mwaka wa pili mfululizo, Tanzania inatoa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa, baada ya mwaka jana Mrisho Khalfan Ngassa kuongoza pia akiwa na klabu ya Yanga SC, kabla ya kuhamia Free State Stars ya Afrika Kusini msimu huu.

Ngassa alifunga mabao sita sawa na El Hedi Belameiri wa Setif, Haythem Jouini wa Esperance na Ndombe Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC, sasa Al Ahly.

error: Content is protected !!