MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema fedha kiasi cha Sh. 4.5 bilioni, zilizotokana na tozo za miamala ya simu, zimejenga vituo vya afya 13 mkoani humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 5 Julai 2022, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT.
“Napenda kukupongeza (Rais Samia), kwa kazi kubwa uliyofanya kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya kwa mkoa wetu wa Dar es Salaam. Nikushukuru kwa kutoa fedha Sh. 4.5 bilioni, kwa ajili ya vituo vya afya,”amesema Makalla na kuongeza:
“Fedha hizi bilioni 4.5 kwa ajili ya vituo vya afya 13, ni hela za tozo za miamala ambayo sasa tumeanza kuona umuhimu wake. Tozo za miamala tumejenga vituo 13. Tukushukuru pia kwa kuboresha afya umetoa Sh. 14 bilioni, kwenye fedha za UVIKO-19, kuboresha vituo vya afya na hospitali za Dar es Salaam.”
Tozo hizo za miamala ya simu, zilianza kutozwa Julai Mosi, 2021.
Leave a comment