MBUNGE wa Viti maalum Dodoma (CCM), Fatma Toufiq, ameahidi kushughulikia changamoto ambazo zinaikabili shule ya msingi maalum ya Buigiri iliyopo Chamwino mkoani Dodoma ikiwemo ujenzi wa ukuta na matibabu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Toufiq aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati Taasisi ya Sauti ya Matumaini (SAMAF) wakikabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo madaftari, taulo za kike, mafuta maalum kwa watoto wenye ualbino, fimbo za wasioona, soski, penseli na kalamu kwa watoto walemavu na wenye mahitaji maalum katika shule hiyo.
Alisema changamoto alizojulishwa shuleni hapo zilizo nje ya uwezo wake atakwenda kuziwasilisha katika mamlaka husika ili zifanyiwe kazi.
Aidha, ameupongeza Umoja wa Wanahabari Wanawake Tanzania (UWWT) chini ya Taasisi ya Sauti ya Matumaini (SAMAF), kwa utayari wao na kuwa mstari wa mbele katika suala la kuisaidia jamii hasa kundi la watoto walemavu na wasiojiweza.
Alisema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanya na serikali ni muhimu kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kuwasaidia watoto hao wenye ulemavu ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.
“Nawashukuru SAMAF kwa upendo wenu mlionao mnafanya kazi kubwa sana ya kurejesha tabasamu na matumaini kwa jamii, sisi Serikali tutaendelea kuzifanyia kazi zile changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili kundi hilo,” amesema Fatma.
Naye Mwenyekiti wa SAMAF, Mary Geofrey alisema lengo la kutoa misaada hiyo ni kurudisha tabasamu kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu na watoto wenye ulemavu ili nao kujiona ni sehemu ya jamii inayothaminiwa na kupewa kipaumbele kama watoto wengine.
“Tunaamini msaada huu utakuwa chachu ya wanafunzi hawa kuongeza juhudi za masomo ili kufikia ndoto na malengo waliyojiwekea bila kujali changamoto zao. Umoja huu ambao tumekuwa tukitumia kalamu kama kiunganishi kati ya serikali na jamii na wadau wengine, tumeamua sasa kujitoa kwa vitendo kuifikia jamii ya makundi maalum kwa nia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea Watanzania wote maendeleo bila kubagua makundi yenye mahitaji,” alisema Mary.
Aidha, Mary alilishukuru Taasisi ya Disability Hope (FHD) kwa kushirikiana nao katika kutoa misaada hiyo na kufanikisha hafla hiyo.
Mtendaji Mkuu wa SAMAF, Penina Malundo, alisema umoja huo utaendelea kusaidia kundi la watoto wenye ulemavu, wasiojiweza na wanaoishi katika mazingira magumu na kuwaomba wadau kusaidia wenye uhitaji.
“Tumefanya jambo hili kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuhakikisha wanafunzi wote wanakuwa na mazingira bora wawepo shuleni hususani katika shule zenye elimu jumuishi. Asante Mbunge Toufiq na uongozi wa Wilaya ya Chamwino pamoja na Shule ya Buigiri kwa kukubali kupokea msaada huu,” alisema Penina.
Leave a comment