May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Toba ya UVCCM yaibua mjadala

Kheri James, Mwenyekiti wa UVCCM

Spread the love

 

HATUA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kuwaomba radhi Watanzania, imewaibua wanasiasa na wanaharakati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Jumapili ya tarehe 28 Machi 2021, Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James, aliwaomba radhi Watanzania kutokana na kauli na matendo yaliyofanywa na umoja huo katika utawala wa Hayati Rais John Magufuli, ambayo yalichochea chuki na uhasama kwa jamii.

Kufuatia hatua hiyo, leo Jumatatu tarehe 29 Machi 2021, baadhi ya wanaharakati, wanasiasa na wananchi wa kawaida wameanzisha mjadala wakiujadili msamaha huo, ambapo baadhi yao waliunga mkono huku wengine wakipinga.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, akizungumza na MwanaHALISI Oniline kuhusu hatua hiyo, amesema ni ya kiungwana kwani inaunga mkono wito wa Rais Samia Suluhu Hassan, wa Taifa kuzika tofauti zao.

“Ni jambo jema na la kiungwana siku zote mtu anayekumbuka alipoteleza na kuomba radhi. Ni uungwana, mimi nadhani sisi kama Watanzania na kama alivyosema Kheri tumsamehe. Na wengine wote waungane na wale wote wanaoomba radhi,” amesema Olengurumwa

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)

“Sababu wote tunajenga Taifa moja. Mama Samia alisema tunajenga Taifa moja na tusiangalie tulipojikwaa bali tuangalie tunakwenda vipi, tusameheane makosa yaliyojitokeza.”

Akilihutubia Taifa tarehe 19 Machi 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Rais Samia alitoa wito kwa Watanzania kuzika tofauti zao, ili wawe wamoja kwa ajili ya kuijenga Tanzania.

Rais Samia aliapishwa kumrithi Dk. Magufuli, aliyefariki dunia akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anaptiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Hilda Newton, kupitia ukurasa wake wa Twitter, ameihoji hatua hiyo akisema kwa nini Mwenyekiti huyo wa UVCCM hakuomba radhi kabla Dk. Magufuli hajafariki dunia.

“Angeomba msamaha wakati Dk. Magufuli hajafa, ningemuelewa ila kuomba msamaha baada ya Dk. Magufuli kufa ni unafiki,” ameandika Hilda, ambaye ni mwenyekiti wa vijana wa Chadema (Bavicha), Temeke.

Naye Katibu wa Kanda ya Pwani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hemed Ali amesema ili msamaha wa Kheri uwe na tija, inabidi uwe na dhamira ya kuliponya Taifa, ili makosa yaliyofanyika awali yasijirudie tena.

Ali amesema ili msamaha huo uwe na tija, iundwe tume huru ya ukweli wa maridhiano itakayochunguza makosa yaliyofanyikwa kwa ajili ya kuwawajibisha wahusika.

Mwanasiasa huyo ameshauri mchakato wa katiba mpya ufufuliwe pamoja na uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.

“Vyombo vya habari viachiliwe huru toka kifungoni kwa takriban miaka 5 na Miezi 5 ilivyokaa. Viweze kuandika na kuchambua mambo kwa ukweli ,uwazi na uhakika,” ameshauri na kuongeza Ali.

“Vyama vya siasa na wanasiasa hasa upinzani kuondolewa katika vifungo vya Mikutano ya Hadhara na Sheria zote kandamizi. Kuachiwa na kufutwa kwa kesi zote za Kisiasa za wanasiasa bila masharti yoyote yale. Bila kusahau kufanya mabadiliko au kufuta kabisa Sheria za Mitandao ya Kijamii.”

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo, Abdul Nondo amesema ngoime hiyo iko tayari kumsamehe Kheri kama UVCCM watajirekebisha.

“Kwa miaka Kheri, tumekuwa tukihubiri kuwa na siasa za upendo na amani ila nyinyi UVCCM mlihubiri chuki waziwazi. Kwaniaba ya Ngome ya vijana ACT-Wazalendo, tumekusamehe kwa sharti la kwamba wewe na vijana wako mnapaswa mjirekebishe,” ameandika Nondo katika ukurasa wake wa Twitter.

Mwanaharakati na Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema UVCCM walishauriwa kutofanya uchochezi lakini hawakusikia, hivyo hatua yake ya kuomba msamaha inahuzunisha.

Maria Sarungi amemhoji, Kheri akisema, amechukua hatua hiyo kwa sababu utawala umebadilika, na kwamba radhi yake hiyo haijatoka moyoni.

“Ni vyema kuomba radhi ila hii siyo kuomba radhi, haikidhi viwango. Unaomba radhi kwa sababu Rais kabadilika lakini kesho akija mwingine anayebagua na kukuza chuki utageuka tena? Hapana Kheri, hujatuomba radhi, bali unataka kutetea masilahi maana upepo umebadilika,” amesema Maria.

Dk. Magufuli alifariki dunia miezi minne tangu, alipoapishwa kuendelea na muhula wake wa mwisho wa uongozi katika Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 5 Novemba 2020, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu.

Mwanasiasa huyo aliiongoza Tanzania katika kipindi cha miaka mitano na miezi mitano (Novemba 2015 hadi Machi 2021). Ambapo alishinda kiti cha urais katika Uchaguzi wa 2015 na 2020.

Mwili wa Dk. Magufuli ulizikwa Ijumaa iliyopita tarehe 26 Machi 2021, nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

error: Content is protected !!