August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TMA yatahadharisha ujio wa ukame, njaa

Spread the love

MAMLAKA ya hali ya hewa hapa nchini (TMA), imewaonya wananchi juu ya ukame na baa la njaa, ambavyo huenda vikalikumba taifa kutokana na kukosekana kwa mvua katika maeneo mengi ya nchi kati ya mwezi Oktoba na Desemba mwaka huu, anaandika Charles William.

Akizungumza na wanahabari leo, Dk. Agness Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA amesema, kutokana na kukosekana kwa mvua kati ya Desemba na Oktoba mwaka huu katika maeneo mengi ya nchi, migogoro baina ya wakulima na wafugaji pia itaongezeka.

“Mvua zinatarajiwa kuchelewa kuanza na zikianza zitakuwa chini ya wastani, wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na pembejeo mapema na wazingatie ushauri wa maafisa kilimo kwa kuwa waangalifu katika kuhifadhi akiba ya chakula waliyonayo,” amesema.

Dk. Kijazi pia ametahadharisha kuwa, huenda kukosekana kwa mvua hizo kukasababisha upungufu wa maji katika mabwawa yanayozalisha umeme na hivyo kuathiri uzalishaji na upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.

“Matukio ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji yanatarajia kujitokeza pia kutokana na uhaba wa maji na malisho kwaajili ya mifugo na hata wanyama pori hivyo mamlaka zinazozunguka jamii husika zijiandae kuchukua hatua stahiki,” Dk. Kijazi amesisitiza.

Utabiri huo wa TMA, umeonyesha kuwa mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro, Kigoma, Rukwa, Katavi na Tabora ndiyo inayotarajiwa kukumbwa na uhaba wa mvua zaidi na hivyo wananchi wa mikoa hiyo wametakiwa kuchukua tahadhari.

Hata hivyo, katika mikoa ya pembezoni mwa Ziwa Victoria, ikiwemo Mwanza, Kagera, Shinyanga, Musoma, Simiyu na Geita pamoja na mikoa ya Kusini mwa nchi, Lindi na Mtwara, mvua zinatarajiwa kuwepo kwa kiwango cha kuridhisha.

Mbali ya ukame na migogoro ya wakulima na wafugaji, TMA imetahadharisha kuwa, athari nyingine ya kukosekana kwa mvua hizo itakuwa ni mlipuko wa magonjwa kutokana na uhaba wa maji salama sambamba na matumizi mabaya ya mifumo ya majitaka katika miji.

Itakumbukwa kuwa, mwezi mmoja uliopita, Rais John Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alitangaza kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa wananchi watakaokumbwa na tatizo la njaa kwa mwaka huu.

error: Content is protected !!