May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TLS waanza kumsaka rais wao

Spread the love

 

WANACHAMA wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), wameanza kujitokeza katika zoezi la upigaji kura kuchagua viongozi wa ngazi za juu za chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Arusha … (endelea).

Zoezi hilo lililoanza majira ya saa 12 asubuhi leo Ijumaa tarehe 16 Aprili 2021, katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), linaendelea hadi saa 4.30 asubuhi litakapofungwa rasmi.

Wanaogombea urais kwenye uchaguzi huo ni Dk. Edward Hoseah, Flavian Charles, Francis Stolla, Shehzada Walli na Albert Msando. Wagombea nafasi ya makamu rais ni Gidion Mandes na Gloria Kabalamu.

Nafasi ya mweka hazina kwenye uchaguzi huo, amejitokeza mgombea  ambaye ni Fredrick Bernard Msumari. Mgombea huyo anatetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Akizungumza baada ya kupiga kura, Dk. Hoseah amesema zoezi hilo linaendelea vizuri.

“Mchakato ni mzuri watu walipata nafasi ya kujinadi na kitoa sera zao kwa wanachama. Mimi sina wasiwasi nitashinda na ikitokea vinginevyo sina wasiwasi sababu sigombei kupata chochote kitu,  nagombea kutoa service (huduma) atakayeshinda nitamuunga mkono,” amesema Dk. Hoseah.

Kwa upande wake Flaviana amesema zoezi la uchaguzi huo linaenda vizuri huku akiwataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi.

“Mchakato uanenda vizuri na hadi siku ya jana ulienda vizuri na naamini leo wanachama watapata nafasi ya kupiga kura. Niwaombe wapiga kura wajitokeze kwa wingi. Naomba watu wapuuze sms kwenye mitandao ya kijamii kwamba nimejitoa, mimi sijajitoa,” amesema Flaviana.

Naye Mandes anayegombea kiti cha Makamu wa Rais, amesema zoezi hilo linaenda vizuri.

“Mchakato uko vizuri, nakubali asilimia mia zoezi limeenda kwa haki na wapiga kura wametimiza wajibu wa kupiga kura,” amesema Mandes.

TLS hufanya uchaguzi wao mkuu kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu watu watano wamejitosa kumrithi Dk. Lugemeleza Nshala, kwenye nafasi ya Urais wa chama hicho.

Dk. Nshala anamaliza muda wake wa uongozi wa miaka mwili (2019-2020), ameongoza kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na TLS kushindwa kufanya uchaguzi mwaka jana, kwa sababu ya marekebisho ya sheria ya chama hicho.

Msando amesema, anaamini mchakato huo utamalizika salama kwa sababu, mpaka kura zinaanza kupigwa, hakuna malalamiko yoyote.

“Bado mchakato unaendelea kuhusu uhuru na haki mpaka tutakapomaliza uchaguzi itajulikana, ila kwa sasa kila kitu kiko sawa.

“Hakuna malalamiko yoyote, naamini uchaguzi utaenda vizuri kwa sababu ni wataaluma Zaidi, sio kama uchaguzi mwingine wa siasa. Sidhani kama unahitaji kutumia nguvu zaidi,” amesema.

error: Content is protected !!