July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Tizeba afumua vyama vya ushirika

Spread the love

CHARLES Tizeba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, amemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Audas Rutambanzibwa, kuvunja Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika (Nyanza) mkoani Mwanza kutokana na matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara serikali, anaandika Moses Mseti.

Bodi hiyo ya ushirika inatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mali za umma, ikiwemo kuuza viwanja na viwanda jijini hapa kwa bei kidogo huku fedha zilizouzwa mali hizo hazijulikani zimefanya kazi gani.

Kiwanja na moja ya kiwanda hivyo, vilivyouzwa na bodi hiyo vina thamani ya zaidi ya Sh. 4 bilioni lakini wao waliviuza kwa Sh. 25 milioni na kwamba, kitendo hicho kimeigharimu serikali.

Akizungumza jana katika kikao na wataalamu wa pamba na bodi hiyo, Tizeba amesema kuwa, kitendo cha bodi hiyo kuuza mali za ushirika huo kunaonesha ni namna gani watu hao waliopewa dhamana ya kusimamia, wasivyokuwa na uchungu na mali za umma.

Tizeba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa mkoani hapa, amesema kuwa kutokana na hali hiyo, imemlazimu kumuagiza msajili wa vyama vya ushirika taifa, kuvunja bodi ya ushirika ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua endapo watabainika na makosa.

Amesema kuwa kutokana na hatua ya bodi kufanya mambo ‘kisani’ na kujilimbikizia mali bila kufuata kanuni na utaratibu, Meneja wa Taaisisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoa wa Mwanza Ernest Makale, kuchunguza suala hilo.

“Wameenda wamekopa benki ya CRDB bilioni 2.2 na wameweka dhamana vitega uchumi vya ushirika ikiwemo jineli 12 za ushirika lakini fedha zilizokopwa hazijulikani zimefanya kazi gani na sasa hivi benki inataka kuuza mali hizo.

“Watu wanafanya mambo wanavyotaka wao na wanakula fedha za ushirika wanavyotaka, sasa Takukuru tunaomba wachunguze mienendo ya bodi hiyo na watakaobainika wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo,” amesema Tizeba.

Hata hivyo kiwanda moja wapo cha ushirika kilichopo karibu na jengo la NSSF kiliuzwa kwa mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Zakari Express, Peter Zakaria ambaye alikinunua kwa milioni 70 badala ya zaidi ya bilioni 2.

Afuta vyama ushirika

Katika hatua nyingine waziri Tizeba, amemuagiza msajili wa vyama vya ushirika Rutambanzibwa, kuvifuta vyama 1860 kati ya 8720 ambavyo havifanyi kazi ili kuendelea na vyama vilivyobaki katika kuviendelez vyama hivyo kwa urahisi zaidi.

Amesema kuwa kusuasua kwa vyama hivyo kunachangiwa na bodi ya vyama hivyo kutokuwa wabunifu wa namna ya utekelezaji wa kazi za kilimo cha pamba pamoja na mrajisi wa Serikali mkoa wa Mwanza, Kija Maeda, kushindwa kusimamia na kutoa ushauri kwa bodi hiyo.

Tizeba amesema kuwa kutokana na hali hiyo, mrajisi wa mkoa huo hapaswi kufumbiwa macho kwani yeye ndo chanzo cha vyama vya ushirika kwa ukanda huo kusimama licha ya wakulima kuonesha mwamko wa kulima zao hilo.

“Lazima tuanze na watumishi hawa wa Serikali ambao wao wameshindwa kutoa hata ushauri kwa bodi na ndo maana wao wamefanya mambo wanavyotaka, kama angekuwa anatoa ushauri mzuri mambo haya tunayoyaona yasingetokea,” amrsema Tizeba.

error: Content is protected !!