October 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Timuatimua ya Magufuli yakumba watatu Mwanza

Spread the love

WATUMISHI watatu wa Halmashauli ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wamesimishwa kazi kutokana na uzembe na uongo ikiwa ni pamoja na kudaiwa kutaka kuidanganya serikali hivyo kuiingia hasara ya shilingi 20 bilioni. Anaandika Moses Mseti … (endelea).

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Meneja wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sengrema, Mhandisi Nestory Kabete; Ofisa Ardhi Wilaya, Richard Pungu na Mkuu wa Kitengo cha Mipango Miji, Wilson James.

Wimbi la watumishi wa umma kusimamishwa kazi limeendelea kuibuka nchini baada ya hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusimamisha kazi watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) Dar es Salaam.

Agizo la watumishi hao kusimamishwa kazi lilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo wakati wa ziara yake mkoani humo ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.

Mulongo amesema watumishi wa umma katika halmashauli hiyo wamekuwa wazembe, waongo na wasiokuwa waaminifu kazini ambapo alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ndalo Kwilijila kuwasimamisha kazi.

Watumishi hao waliingia kwenye makosa baada ya awali kumueleza Mulongo kuwa, mradi wa maji unaotekelezwa na kampuni ya kichina ya Cowi, umeshindwa kuendelea kutokana na bomba la maji kupita katika nyumba ya Pamphil Masashua.

Baada ya maelezo hayo Mulongo aliomba kupelekwa katika mradi huo, walipofika katika eneo hilo watumishi wote watatu walishindwa kuthibitisha kama bomba hilo limepita kwenye nyumba hiyo.

Kufuatia hatua hiyo ya watumishi hao kushindwa kuthibitisha ukweli huo, Mulongo alimtaka Katibu Tawala huyo kuwapa barua za kusimamishwa kazi kutokana na uzembe na uongo wa wazi wazi waliouonesha.

“Kuna watumishi wachache ambao wamekuwa waongo, wanashindwa kutambua kama wao ni sehemu mojawapo ya serikali wanakaa wanapanga mipango na watu kwa lengo la kuingiza serikali hasara, sasa wasimamishe ili wajifunze.

Mulongo amesema watumishi hao wamekuwa chanzo katika jamii kuichonganisha serikali na wananchi kuona kwamba haifanyi kazi kwa bidii.

Awali akijizungumzia suala la mradi huo kupita katika nyumba hiyo, Meneja wa Maji safi na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Nestory Kabete, amesema yeye hahusiki na suala hilo kwani ni mgeni katika utumishi kwenye wilaya hiyo.

“Mkuu (Magesa Mulongo) mimi ni mgeni, sina muda mrefu kuna wengine ambao walikuwepo na pia wakati mradi huu unapita hapa uliikuta nyumba hii ikiwepo,” amesema Kabete.

error: Content is protected !!