TIMU ya Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CMT), imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mkonze. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Kauli hiyo ilitolewa na Shaban Juma, mwenyekiti wa timu hiyo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi unaoendelea wa kituo hicho kilichopo katika Kata ya Mkonze.
Juma amesema kuwa, ujenzi huo unaenda vizuri kwa mujibu wa ratiba ya kazi iliyopo na kuwa, matarajio ya timu hiyo ya uongozi ujenzi huo utakamilika ifikapo tarehe 16 Julai 2019.
Juma amesema kuwa, maeneo ya mipaka ya kituo hicho cha afya yabainishwe na kuwekewa alama ili kuepuka uvamizi na makazi holela katika eneo la kituo hicho.
Utambuzi na uwekaji wa mipaka ya kituo hicho utasaidia kuondoa migogoro na wananchi, hasa kituo hicho kitakapohitaji upanuzi.
Maelekezo mengine yaliyotiliwa mkazo ni kuongeza kasi ya utaratibu wa manunuzi ya milango 50 ukamilike na kupachikwa ili kuruhusu taratibu nyingine za ujenzi wa ndani ziweze kuendelea.
Vilevile, uongozi wa kituo hicho cha afya ulielekezwa kufanya usafi wa mazingira ili kuboresha mandhari ya kituo hicho.
Awali Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk. Baraka Chaula alisema kuwa, serikali ilitoa kiasi cha Sh. 400 milioni kwa ajili ya upanuzi wa kituo cha afya Mkonze.
Maelekezo hayo aliyataja kuwa ni ujenzi wa jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi.
Leave a comment