‘TIKI Taka mpaka kwa Mkapa,’ ndio kauli mbiu wanayoingia nayo klabu ya Simba kwenye mchezo wa marudiano wa klabu bingwa barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Plateau kutoka nchini Nigeria. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Mchezo wa mzunguko wa kwanza ulichezwa kwenye mji wa Jos, Nigeria, Simba waliibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lilifungwa na kiungo wake kimataifa kutoka Zambia, Cloutous Chama.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi tarehe 5 Novemba, 2020, majira ya saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam huku ukiruhusiwa kutazamwa na mashabiki 30,000 tu.
Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa siku ya mchezo huo watakwenda na kauli mbiu ya ‘Tik Tak’ lengo sio kupata ushindi tu, bali kucheza mpira mzuri ambao utawaburudisha mashabiki wa klabu hiyo.
“Tunakwenda kuwaburudisha mamilioni ya watanzania kwenye Uwanja ambao kwetu ni machinjio kwa wageni wetu, hatuendi kucheza tu, tunakwenda na burudisha na wala hatuwadharau, Plateau ingawa tumewafunga kwenye mchezo uliopita,” alisema Manara.
“Hatuendi kucheza michuano hii kama hisani, tunakwenda kucheza kama mabingwa mara baada ya kuchukua ubingwa wa msimu uliomalizika kwa hiyo lazima tuwakilishe nchi kwenye mashindano ambayo tumeyataka” aliiongezea Haji Manara
Tiki Taka ni aina mpira wa kihispania ambao sifa yake kubwa ni kumiliki mpira kwa kupiga pasi fupi fupi huku timu ikiwa inatembea kwenda kushambulia na mara nyingi aina hii ya mpira hutumika na klabu ya FC Barcelona ya Hispania.
Simba inaingia kwenye mchezo huo wa marudiano siku ya Jumamosi huku ikiwa na kumbukumbu ya kuondoshwa kwenye michuano hii katika hatua ya awali kwenye msimu uliopita dhidi ya UD Songo kutoka Msumbiji mara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Viingilio kwenye mchezpo huo vitakuwa Tsh. 150,000 kwa Platinum, VIP A Tsh. 40,000, VIP B na C Tsh. 20,000 huku mzunguko ikiwa ni Tsh. 7,000.
Leave a comment