July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tiba ya moyo yafanyika kisayansi zaidi

Jengo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

Spread the love

TANZANIA imeandika historia nyingine leo, baada ya kufanya tiba ya Moyo bila kufanya upasuaji kwa kuziba matundu yaliyopo kwenye moyo kwa kutumia kifaa maalumu kiitwacho Stent, pasipo kufungua kifua kama ilivyozoeleka. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Tiba hii imefanyika kwa mara ya kwanza nchini  kupitia idara ya tiba  na upasuaji Moyo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikishirikiana na madaktari bingwa kutoka  Hospitali ya Prince Sultani Cardiac iliyopo Riyadhi nchini Saud Arabia.

Akizungumza na waandishi ofisini kwake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Hussein Kidanto, amesema, madakitari hao watakuwepo hospitalini hapo kwa siku 9, kuanzia Mei 8 hadi 16 mwaka huu.

Dk.Kidanto amesema, madaktari hao wamekuja kupitia Taasisi ya Al Mutanda Islami Trust ya Uingereza, ambapo jumla ya wagonjwa 20 wanatarajiwa kupatiwa tiba hiyo.

Amefafanua kuwa, Aprili mwaka huu, walifanya majaribio kwa kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye Moyo na kuweka kifaa maalumu (Stent), ambapo mtambo maalumu wa Cath Lab unatumika baada ya kufanya uchunguzi wa kuangalia mishipa ya damu inayoenda kwenye moyo, jinsi unavyofanya kazi, na kama kuna mshipa umeziba uweze kuzibuliwa.

Amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwezi uliopita, jumla ya wagojwa 31 walifanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na wagojwa 4 waliweza kuzibuliwa na mishipa yao ya moyo kuwekewa Stent ambapo damu iliweza kupita.

“Kasi hii ya utoaji wa huduma hizi inatarajia kuleta tija kwa wagojwa wenyewe, Taifa na wauguzi. Huduma hizi mbili kuanzia uchunguzi hadi matibabu hazijawahi kufanyika popote nchini isipokuwa hospitalini hapa.

“Kwa misingi hiyo basi, Tanzania imeandika historia ya kipekee, na huenda kasi ya kupeleka wagojwa nje ikapungua,” amesema Kidanto.

Aidha, amesema, moja ya malengo yao ni kuhakikisha wanashirikiana na taasisi za kitaaluma rafiki na kuwakaribisha kuja kufanya nao kazi, na hivyo kujenga uwezo hapa nchini kwa watu wengi zaidi.

“Taaluma ya matibabu inabadilika kwa kasi kubwa sana duniani na ili Muhimbili iweze kwenda sambamba na kasi hiyo ni lazima kufanya ushirikiano na nchi ambazo zimepiga hatua kubwa kwenye  nyanja mbalimbali za matibabu ili na sisi tuweze kujitegemea,” amesema.

error: Content is protected !!