December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC:Marekebisho ya sheria za habari yataiheshimisha TZ kimataifa

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Spread the love

MCHAKATO wa marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya habari nchini, umetajwa kuirudisha heshima ya Tanzania kimataifa, katika masuala ya ulinzi wa uhuru wa kujieleza, haki ya kutoa na kupata taarifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa jana Jumapili, tarehe 30 Oktoba 2022 na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.

Olengurumwa amesema, mchakato huo ukikamilika utaiweka Tanzania katika mazingira mazuri ya kuheshimu haki hizo za binadamu, huku akiipongeza Serikali kwa kutunga muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kwa kuwa ni hatua itakayotokomeza changamoto ya udukuzi wa taarifa.

“Maboresho ya sheria za habari na kuongeza sheria iliyokuja sasa hivi ya Data Protection inayohifadhi taarifa zetu zisiingiliwe kirahisi, nadhani zote kwa pamoja zitakwenda kuweka mazingira mazuri kwamba Tanzania ni nchi inayoheshimu na kulinda misingi ya uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari, haki ya kupata na kusambaza taarifa. Nadhani tukifanya hivyo tutapiga hatua kubwa sana,” amesema Olengurumwa.

Hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, atakutana na wadau wa sekta ya habari kwa ajili ya kupitia tena mapendekezo yaliyotolewa kuhusu marekebisho ya sheria hizo.

Msigwa alisema Nape atakutana na wadau hivi karibuni ili kupitia kwa mara ya mwisho mapendekezo hayo, kwa lengo la kupatikana sheria zinazokubalika na pande zote.

error: Content is protected !!