December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC yazindua mtandao wa kuhifadhi data na kushirikisha taarifa

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umezindua mtandao wake wa usajili, ufuatiliaji na usimamizi wa wanachama wake zaidi ya 200 Tanzania bara na visiwani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo wa kidigitali, leo Alhamisi, tarehe 29 Septemba 2022, jijini Dar es Salaam, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema utasaidia kuongeza ukaribu kati ya mtandao huo na wanachama wake, pamoja na kuokoa muda na kuachana na matumizi ya nyaraka ngumu.

“Tunategemea wanachama wote wataona shughuli zote za THRDC kupitia mtandao huu ambao utakuwa kama kituo cha pamoja kati ya THRDC na wanachama.Mtu anayetaka kujua watetezi wa haki za binadamu wanafanya nini, akiingia kwenye mtandao ataona wanachama wetu wanavyofanya kazi na mahali yanakopatikana,” amesema Olengurumwa.

Afisa Mkuu wa Dawati la Wanachama THRDC, Lisa Kagaruki, amesema kupitia mtandao huo, wadau wa masuala ya utetezi wa haki za binadamu wakiwemo wafadhili kutoka nje ya nchi, watapata nafasi ya kujua viongozi wa kanda 11 za mtandao huo, zilizoko Tanzania Bara na Zanzibar.

“Kupitia mtandao huu, tutaweza kuwajua viongozi wa kanda, wadau wanapotaka kutembelea wanachama watawapa viongozi wa kanda kwa ajili ya kupanga mipango ya kuzitembelea kanda hizo,” amesema Lisa.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Bluefin Solution Limited, ambayo imetengeza mtandao huo unaojuliakana kama THRDC Data Base, Mussa Kisena, amesema kuanzia sasa mtandao huo, pamoja na wanachama wake, watapata nafasi ya kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo.

Amesema, watumiaji wa mtandao huo watapata nafasi ya kupakia na kupakua nyaraka mbalimbali na kuchapisha taarifa zao, huku akiwahakikisha kwamba una usalama wa uhakika.

“Mfumo huu umetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, katika hilo tumeweza kuhakikisha mambo yote ya kiusalama ikiwepo ya data na mfumo yamezingatiwa. Tumeiweka katika mazingira ambayo yana kiwango kikubwa cha usalama katika mfumo wa usalama wa kimataifa, hivyo hakuna namna wadukuzi wakauingilia,” amesema Kisena.

error: Content is protected !!