May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC yawanoa wanachama wake, yawapa masharti

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania (THRDC), umefanya semina ya kuwajengea uwezo wanachama wake wapya 70. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Semina hiyo ya siku mbili kuanzia leo Jumanne na kesho, tarehe 30 Juni 2021, imefanyika jijini Dar es Salaam.

Ni maandalizi ya maadhimisho ya saba ya siku ya watetezi wa haki za binadamu Tanzania, yatakayofanyika tarehe 2 Julai 2021, katika ukumbi wa Mlimani City mkoani humo.

Akizuingumza katika semina hiyo, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema, wamefanya semina hiyo ili kuwafundisha wanachama hao sera, misingi na mambo yanayotekelezwa na mtandao huo.

“Semina hii ipo kwa malengo mazuri kabisa, kwanza wewe mwenyewe tukufahamu lakini pia na wewe uufahamu mtandao na misingi yake. Lengo ni kuwasaidia kufahamiana, mtandao unawasaidia kuwaleta pamoja, tuitumie hii fursa vizuri ,”amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amewasisitiza wanachama hao wapya kuendelea kufanya vizuri katika kazi za utetezi wa haki za binadamu ili mtandao huo uendelee kutoa mchango mzuri kwa wananchi nchini.

“Msingi mkubwa na kigezo kikubwa cha kuwa mwanachama hapa ni kutetea haki, ukiacha kutetea haki maana yake ni uanachama wako unaanza kuwa kwenye shida, unaanza kutushawishi uongozi uone kwamba ulikosea kukusajili kuwa mwanachama,” amesema Olengurumwa.

Aidha, Olengurumwa amewataka wanachama hao, kuweka kumbukumbu za kazi za utetezi wa haki za binadamu wanazofanya.

“Jitahidini kuweka kumbukumbu vizuri na ndiyo maana tukaanzisha utaratibu na huu ni utaratibu wa lazima ukishakuwa mwanachama wetu kila mwaka utume taarifa ya kazi mnazozifanya na sio lazima usubiri mwaka uishe,” amesema Olengurumwa.

error: Content is protected !!