May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC yalia na changamoto za kodi, TRA yajibu

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu Taifa

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeiomba Serikali iondoe changamoto za kikodi zinazokabili Asasi za Kiraia nchini (Azaki). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi, tarehe 1 Julai 2021 na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, katika semina ya kuwajengea uwezo wanachama 150 wa mtandao huo, kuhusu masuala ya kodi, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City mkoani Dar es Salaam.

Olengurumwa amesema, changamoto kubwa inayokwamisha Azaki nchini, ni kupata kibali cha kujiendesha kama taasisi za kimsaada na kuiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutoa vibali kwa asasi zinazofanya kazi za kijamii.

“Suala lingine gumu kwa asasi ilikua kupata ile hadhi ya kuwa taasisi za kimsaada, ambayo ukiangalia hata tafsiri yetu asasi za kiraia nyingi zinafanya kazi za kijamii, ile hadhi ya kuwa taasisi ya msaada utaratibu wake wa kuipata imekuwa mgumu,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa ameongeza “Asasi mpaka ufanyiwe uthibitisho inakuwa shida na wakati mwingine ukikuta maafisa hawaelewi kazi zetu au sekta zetu, unafanya maombi unadondokea kwake huku haijui sekta, inakuwa ngumu sana kupata.”

Wakati huo huo, Olengurumwa ameiomba Serikali kupitia TRA, isamehe malimbikizo ya madeni ya kodi ya Asasi hizo.

“Tunaomba tufikiriwe katika mzingira tofauti ikizingatia kwamba asasi hazina fedha inazotengeneza, ni fedha za wahisani. Kama kuna madeni yapo zipewe msamaha wa riba na kodi, ili waweze kulipa,” amesema Olengurumwa.

Mratibu huo wa THRDC amesema, changamoto hiyo inasababisha asasi kukosa misaada kutoka kwa wafadhili, kwa kuwa hutozwa kodi nyingi katika vifaa vya misaada inazopata.

“Ukiweka mazingira magumu ya kupata hadhi ya kimsaada, itafanya watu ambao walipaswa kupata misamaha ya kuingiza vifaa kutoka nje baadhi ya kodi watakosa. Lakini kutokana na utaratibu mgumu wa kisheria ambao umeweka mazingira magumu kupata,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa ameiomba Serikali iondoe tozo ya mafunzo na maendeleo ya ufundi stadi (SDL), kwa asasi hizo.

“Asasi za kiraia zinalalamikia baadhi ya kodi, mfano tozo ya SDL, wanaona wasingepewa kutokana na mfumo wetu wa kufanya kazi. Sababu kazi zetu ni za msaada, kuisaidia jamii kwa kupata fedha za wafadhili na wahisani kutoka nje,” amesema Olengurumwa.

Pia, Olengurumwa ameiomba Serikali iondoe makato ya malipo ya mwezi ya mapato yatokanayo na ajira (PAYE), kwa asasi za kiraia kwa kuwa hazijiendeshi kibiashara, hupata fedha kutoka kwa wafadhili.

“Asasi za kiraia tunajua mfumo wetu wa kazi ni wa kupata hela kutoka kwa wafadhili, sasa mfadhili anakupa hela ya mshahara hayo mambo mengine ya kulipia vitu vingine utajua mwenyewe. Utaona unakatwa PAYE na yeye anaona hela anayokupa tayari imeshakatwa kodi,” amesema Olengurumwa na kuongeza:

“Nchi yetu imeshaingia makubaliano na nchi nyingine kuhusu masuala ya kodi, vitu vingine visilipiwe kodi mara mbili sababu tayari hela inayokuja kule ni ya walipa kodi wa nchi zingine, wanakuja kutusaidia. Sisi sio wafanyabiashara, uwezekano wa kupata hela sio wa uhakika.”

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo

Akijibu changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, amezitaka asasi hizo kuwasilisha changamoto zao Serikalini, ili zifanyiwe kazi.

“Nawasihi wadau wote wanapoona kuna haja ya kuboresha mazingira ya kisheria, kisera na taratibu msisite kutoa mapendekezo yenu kwetu. TRA na Wizara ya Fedha tutashughulikia mapendekezo muhimu mtakayoleta kwetu,” amesema Kyombo.

Kayombo amesema, Serikali kupitia TRA inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa asasi hizo kulipa kodi.

“TRA itaendelea kushughulikia changamoto zote kwa kushirikiana na mamlaka husika za Serikali na Serikali inaahidi mazingira ya ulipaji kodi yatendelea kuwa mazuri zaidi,” amesema Kayombo na kuongeza:

“Sisi TRA mambo mengi ambayo yamekuwa yanaletwa kwetu tumeyafanyia kazi na naamini kabisa hatua ya leo ina lengo kuhakikisha tunatatua changamoto katika sekta yenu ambayo huko nyuma tulikuwa na mivutano lakini sasa tunaelekea vizuri.”

error: Content is protected !!