May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THRDC: Vyama vya siasa vijifunze TLS

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu Taifa

Spread the love

 

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeishauri Serikali nchini humo na vyama vya siasa, kuiga mfano wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), jinsi kilivyoendesha michakato ya chaguzi zake. Anaripoti Regina Mkonde, Arusha … (endelea).

Ushauri huo umetolewa jana Ijumaa, tarehe 16 Aprili 2021, na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, akizungumza na wanahabari jijini Arusha.

TLS kilifanya uchaguzi wake mkuu jana Ijumaa katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ambapo Dk. Edward Hoseah, aliibuka mshindi wa nafasi ya urais, kwa kuwashinda wenzake wanne.

Olengurumwa amesema ni mfano wa kuigwa kwa serikali na vyama vya siasa kwa kuwa mchakato wake ulikuwa wa huru na haki.

“Uchaguzi wetu wa chama, mara zote umekuwa ukizingatia taratibu za uhuru wa uchaguzi, kuanzia zoezi la wagombea kuteuliwa, watu wanaostahili kuchaguliwa wanapita bila shida. Hatujaona mambo yaliyojitokeza katika chaguzi nyingine za kisiasa,” amesema Olengurumwa.

Dk. Edward Hoseah, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Nchini Tanzania baadhi ya vyama vya siasa, vimekuwa vikilalamikia michakato ya uchaguzi kuwa na dosari, ikiwemo baadhi ya wagombea wake kutoteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mawakala wake kutolewa nje ya vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, Serikali na NEC imekanusha madai hayo ikisema mchakato wa uchaguzi nchini huendeshwa kwa haki na usawa.

“Uchaguzi huu umetoa mfano wa namna chaguzi zinavyoendeshwa, watu wanafanya kampeni za sawa na haki. Vyombo vya habari vimetoa nafasi kwa wote, ni moja wapo ya uchaguzi mzuri kama tutaweza kuiga katika chaguzi nyingine zingesaidia kama Taifa,” amesema Olengurumwa.

Wakili Peter Kibatala, akipiga kura katika uchaguzi Mkuu wa chama hicho

Uchaguzi huo wa rais, makamu wa rais na mweka hazina wa TLS, umefuatiliwa na Watanzania wengi ndani na nje ya nchi, ambapo Olengurumwa amesema, hali hiyo inasababishwa na mchango mkubwa wa chama hicho katika kuimarisha utawala wa sheria na kusaidia jamii.

“TLS ni chama muhimu katika kulinda maslahi ya umma, ndiyo manaa leo Watanzania wote masikio yao yako hapa tofauti na chaguzi za taaluma nyingine.”

“Uchaguzi wao unatoa mfano kwa umma kwa sababu chaguzi zote zinapaswa kuendeshwa kwa uwazi,” amesema Olengurumwa..

Amesema “Wanasheria wana jukumu la kusaidia jamii katika majukumu makubwa manne ya TLS, mfano majukumu kwa mahakama na jamii. Muda wote wanasheria na chama hiki wamekuwa wakifanya mambo yanayohusu wananchi.”

Akielezea majukumu ya TLS kwa jamii, Olengurumwa ambaye naye ni wakili amesema, chama hicho kimekuwa kinatoa ushauri kwa Serikali, Mahakama, Bunge na jamii kwa ujumla pale panapotokea masuala mbalimbali yanayohusu utawala wa sheria.

Dk. Rugemeleza Nshala, Rais wa TLS aliyemaliza muda wake, akipiga kura katika uchaguzi Mkuu wa chama hicho

Pia, kimekuwa kikitoa msaada maeneo yenye maslahi kwa jamii.

Katika uchaguzo huo uliosimamiwa na Charles Rwechungura, Dk. Edward Hoseah alitangazwa mshindi wa kiti cha urais huku nafasi ya makamu wa rais ikichukuliwa na Gloria Kalabamu .

Dk. Hoseah alishinda kwa kura 293 kati ya kura 802 zilizopigwa na mawakili walioshiriki uchaguzi huo.

Dk. Hoseah aliyewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru), nchini Tanzania, aliwashinda wagombea wenzake wanne, Flaviana Charles aliyepata kura 223, Francis Stolla (17), Shehzada Walli (192) na Albert Msando (69).

Viongozi waliochaguliwa, wanaapishwa leo Jumamosi, ili kuanza kutekeleza majukumu yao kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na Dk. Hoseah, anachukua nafasi ya Dk. Rugemeleza Nshala aliyemaliza muda wake wa uongozi.

error: Content is protected !!