MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN), wamelaani tukio la kupigwa kwa Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Jesse Mikofu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Tukio hilo limetokea leo Jumatano tarehe 21 Aprili 2021, visiwani Zanzibar, ambapo Mikofu anadaiwa kushambuliwa na Askari Polisi wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wakati akitekeleza majukumu yake.
Mwandishi huyo alikumbwa na mkasa huo, wakati akipiga picha baadhi ya askari waliokuwa katika majukumu ya kuwahamisha wamachinga waliopanga bidhaa zao barabarani katika eneo la darajani.
Akizungumzia sakata hilo, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa ametoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua askari wanaotuhumiwa kufanya tukio hilo.
“Tuna laani tukio hilo na kuomba vyombo vinavyohusika kuona namna gani za kuwachukulia hatua za kisheria askari hao na mwandishi arudishiwe vifaa vyake, vikosi hivyo vihusike kugharamia matibabu yake kama wamemjeruhi,” amesema Olengurumwa.

Salome Kitomari, Mwenyekiti wa MISA-TAN amelaani tukio hilo akisema, kama mwanahabari huyo alitenda kosa ilipaswa achukuliwe hatua za kisheria badala ya kupigwa.
“Ikumbuke kuwa waandishi wa habari wanatekeleza wajibu wao kisheria, na katika utekelezaji wa majukumu yake tunaamini hakuvunja sheria yoyote na kama alivunja sheria utaratibu wa kisheria ungechukuliwa dhidi yake na siyo kumuhukumu kwa kipigo na kuharibu vifaa vyake,” amesema Kitomari na kuongeza:
“Tunaamini SMZ itachukua hatua madhubuti dhidi ya askari waliotenda kosa hilo linalominya uhuru wa upatikanaji taarifa kwa mujibu wa sheria ya Access to Information Act 2016, na uhuru wa kujieleza.”
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema taarifa hizo hazijamfikia na kuahidi kuzifanyia kazi pindi atakazozipata.
Leave a comment