August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘The Great Dar’ kuanza kung’ara

Spread the love

JIJI la Dar es Salaam linaloongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), sasa litaanza kung’ara, anaandika Regina Mkonde.

Halmashuri ya Manispaa ya Ilala imeanza kufungua mlango kwa kukabiliana na kampuni zinazofanya kazi kwa kuvizia ikiwa ni pamoja na kukagua vifaa vya usafi kwa kampuni hizo mara kwa mara ili kufikia lengo hilo.

Ni baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu Jiji la Dar es Salaam kukithiri uchafu ambapo halmashauri hiyo imeanza ‘kupiga mbio’ ili kuondoka kwenye fedheha ya uchafu,

Isaya Mngurumi, mkurugenzi wa halmashauri hiyo amesema, mikataba ya kampuni za usafi zilioingia zabuni na halmashauri hiyo itasitishwa iwapo wamiliki wake watashindwa kutekeleza matakwa yote.

Akizungumza na wakurugenzi wa kampuni za usafi wakati akikagua vitendea kazi vya usafi vya kampuni hizo leo Mngurumi amesema, atahakikisha anafanya ukaguzi kila mara ili kubaini kampuni zisizotekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Kampuni nyingi zimezoea kufanya ujanja ujanja, katika mikataba wanaahidi vingine na utekelezaji wake unakuwa vingine.

“Nitakagua ufanyaji kazi wenu kila mara ili nibaini kampuni zisizofanya kazi inavyostahili,” amesema Mngurumi na kuongeza;

“Ukiangalia maelezo yao katika mikataba yanaonesha yanakidhi matakwa yetu lakini ninataka kujiridhisha kama kweli kazi zinafanyika kulingana na maelezo waliyoyatoa wakati wa kukabidhiwa tenda.”

Ameeleza kuwa, kila mtaa kupitia mwenyekiti wa wake wa mtaa utawasilisha taarifa za kila siku kama kampuni husika katika eneo hilo imefanya kazi yake ikiwemo ukusanyaji wa taka ili wasipofanya hivyo halmashauri ipate taarifa na kuwafanyia kazi.

“Kutakua na ukaguzi kila siku, gari isipopita kwa siku kadhaa tunataka tujue sababu zilizopelekea kutopita, na kama gari litapata hitirafu mmiliki inabidi atoe taarifa na kuchukua gari linguine ili liendelee na kazi,” amesema.

Mngurumi amesema, Halmashauri ya Ilala itahakikisha inaweka mazingira safi ili kuepuka magonjwa ya milipuko hasa kipindupindu.

Tabu Shaibu, Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala amesema, lengo la kufanya ukaguzi ni kuhakikisha kwamba kampuni zinakuwa na vitendea kazi vya kutosha ili kurahisisha kazi za ufanyaji usafi.

“Tunakagua vitendea kazi vyao ikiwemo vifaa vya usalama na magari ya kuzolea taka kama vinatosha kulingana na mahitaji ya eneo husika,” amesema Tabu.

Joha Lemki, Mwenyekiti wa Mtaa wa Fire amesema, kampuni inayofanya usafi mtaani kwake inatekeleza majukumu yake lakini changamoto ya miundombinu imekuwa sababu ya kukwama kwa shughuli za usafi.

“Kila Jumatano na Jumamosi gari linapita kuzoa taka mtaani kwangu, wanajitahidi kutekeleza wajibu wao lakini kinachowakwamisha wakati mwingine ni ubovu wa miundombinu,” amesema Lemki.

error: Content is protected !!