January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THBUB: Tanzania isaidiwe mauaji ya Albino

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi ya kutatua mauaji ya albino nchini

Spread the love

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wameiomba Jumuiya ya kimataifa kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika mapambano yake dhidi ya ukatili na mauaji ya watu wenye ualbino, kwa kuipatia fedha na misaada ya kiufundi. Anaandika Sarafina Lidwino…(endelea).

Ombi hilo lilikuja baada ya THBUB kukutana na wadau wa haki za binadamu, zikiwemo taasisi za serikali, asasi za kiraia vikiwemo vyama vya watu wenye ualbino, taasisi za kidini na washirika wengine kutoka umoja wa mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga amesema, katika mkutano huo wadau wote kwa pamoja  walikemea ukatili huo unaofanywa na watu wenye imani za kishirikina dhidi ya Albino.

Nyanduga amesema katika majadiliano yao walikubaliana kuwa, mapambano dhidi ya ukatili huo ni suala mtambuka, linalohitaji rasilimali fedha za kutosha na jitihada za pamoja ili kufanikisha.

“Tumeamua kuomba serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya taasisi za serikali zinazohusika na suala hili, kutekeleza majukumu yao katika kuelimisha jamii juu ya ukatili huu.

“Inaonekana utekelezaji unakuwa hakuna kutokana na ufinyu wa fedha za kuwawezesha katika ufuatiliaji,”amesema Nyanduga.

Ametaja mapendekezo ya wadau hao katika kukomesha ukatili huo kuwa ni idara ya mahakama kuharakisha usikilizaji wa kesi za mauaji ya Albino, ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka (DPP) iainishe masuala ya mashitaka dhidi ya wauaji wa Albino yapewe kipaumbele.

Ameongeza kuwa idara ya uhamiaji itekeleze kikamilifu sheria ya uhamiaji na iwabaini waganga wa jadi wanaotoka nje ya nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ziimarishe ulinzi kwa watu wenye ualbino na madhehebu ya dini waendelee kutao ushauri na mafundisho yenye kujenga na kukemia kuhusu mauaji hayo.

“Kwa niaba ya wadau wenzangu nitoe wito kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mapendekeso haya yanatekelezwa. Pia niwashukuru wale wote ambao wameendelea kuchukua hatua mahsusi za kupambana na ukatili huu,” amesema Nyanduga.

error: Content is protected !!