January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

THBUB: CUF walidhalilishwa

Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akipigwa na polisi wakati wa maandamano

Spread the love

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa ripoti ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi kuwapiga na kuwadhaliliaha viongozi na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF). Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti  THBUB, Bahame Nyanduga amesema “Tumebaini kuwa, Jeshi la Polisi lilitumia nguvu na kusababisha majeraha kwa kutumia mabomu ya machozi. Lilikiuka misingi ya utawala bora, walivunja haki za binadamu na udhalilishaji dhidi ya mwanachama wa kike.”

Nyanduga amefafanua kuwa, kwa upande wa CUF, walibaini kuwa wana kikundi cha ulinzi cha Blue Guard, ambacho kiko kinyume cha sheria.

Amesema “27 Januari mwaka huu, tume ilipata taarifa kupitia vyombo vya habari zikionyesha jeshi la polisi wakiwapiga na kuwakamata watu waliokuwa kwenye msafara wa Mwenyekiti wa CUF,  Prof. Ibrahim Lipumba.”

Kwamba, tukio hilo lilitokea katika eneo la Mtoni mtongani, Wilaya ya Temeke, ambapo wafuasi hao waliongozana na Prof.Lipumba kutuliza fujo za wanachama wa CUF eneo hilo.

Nyanduga amesema, walianza uchunguzi wao Februari 3 hadi Mei 15 mwaka huu, wakiwa na lengo la kuchunguza kama taratibu mbalimbali zilifuatwa na iwapo kama haki za binadamu zilivunjwa au misingi ya utawala bora ilikiukwa.

Ameeleza kuwa, kutokana na tuhuma hizo, THBUB ilizingatia matakwa ya kifungu cha 130 (1) (c), (f) na (g) cha katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kifungu cha 6(1) (c) na (g) vifungu 15(1) (a) na 28(1), (b) na (f) vya sheria ya THBUB Na.7 ya mwaka 2001, sheria ya Polisi wasaidizi, sura ya 322 na sheria ya Vyama vya Siasa, sura 258.

Aidha, THBUB imetoa mapendekezo kwa taasisi mbalimbali za Serikali na vyama vya siasa kwamba, Jeshi la Polisi lizingatie haki na sheria za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yake. Maafisa wa Polisi wapewe mafunzo mbalimbali yahusuyo haki za binadamu, lizingatie uhuru wa vyombo vya habari.

“Kwa upande wa CUF tumependekeza kuwa, kitafute namna ya kuboresha mahusiano yake na Jeshi la Polisi na kuepuka udhalilishaji katika shughuli za kisiasa, pia kizingatie sheria za nchi na ibara ya 147 (1) ya Katiba ya mwaka 1977, inayozuia Chama chochote kuwa na kikundi chenye mtazamo wa kijeshi.

error: Content is protected !!