October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TGNP: Jamii ishiriki kudhibiti ukeketaji

Spread the love

IKIWA imebaki siku moja kufikikia siku ya maadhimisho ya kupinga ukeketaji duniani (6 Februari 2016), mwakilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Grace Kisetu ameeleza kuwa, lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kuileta jamii pamoja katika kujadili hali ilivyo, kutambua changamoto na kutafuta njia nzuri za kukabilina na tatizo la ukeketaji. Anaandika Sarafina Lwidino.

TGNP jana jijini Dar es Salaam ilifanya majadiliano yaliyowashirikisha wananchi mbalimbali, viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa dini na vyama vya siasa pamoja na waandishi wa habari lengo likiwa ni kuweka mikakati ya kupambana na ukeketaji.

“Takwimu za mwaka 2010 zinaonesha kuwa, takribani asilimia 15 ya wanawake Tanzania wamekeketwa hivyo mnaweza kuona bado tuna kazi kubwa kwani vitendo hivyo vinaendelea,” Amesema Kisetu.

Amsesema pamoja na Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayomlinda mwanamke pamoja na kutunga Sheria Namba 16 ya Kanuni za Adhabu ambayo inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu hadi 15, bado vitendo vya ukeketaji vinaendelea nchini.

Alitaja mikoa inayoongoza katika ukeketaji ikiwa ni pamoja na Manyara (asilimia 71), Dodoma (asilimia 64), Arusha (asilimia 59), Singida (asilimia 51), Mara (asilimia 40), Morogoro (asilimia 21) na Tanga (asilimia 20).

Akiwasilisha shughuli zinazofanywa na Kikundi cha Sauti ya Wananchi Kipunguni katika kupambana na ukeketaji katika kata hiyo, Mwenyekiti wa kikundi hicho Seleman Bishagazi amesesema, kitendo hicho kimekuwa kikifanyika kwa siri kubwa.

Amesisitiza kuwa, baadhi ya familia za makabila yanayofanya ukeketaji katika eneo hilo huwafanyia ukeketaji watoto wao punde tu wanapozaliwa hivyo kuongeza changamoto zaidi.

Diwani wa Kata ya Kipunguni, Mohamed Msofe aliahidi kutafuta ofisi kwa ajili ya kikundi hicho ili kiweze kufanya shughuli za harakati kwa ufanisi zaidi hasa katika kuleta maendeleo.

”Nawaomba viongozi wa dini, waalimu na wanaharakati kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu na anawahimiza Sauti ya Wananchi Kipunguni kutoa elimu kuhusu ukeketaji kwa njia ya sanaa katika mikutano ya wananchi,” amesema Msofe.

Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Kituo cha Polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga, Lydia Mrema amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa na ushahidi ili haki iweze kutendeka.

‘Ushahidi ndio unaomtia mtu hatiani, lakini changamoto ni kuwa ushahidi unakuwa hafifu kwani wahusika huwa wanafamilia” amesisitiza Lydia.

error: Content is protected !!