December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TGDC kuzalisha megawati 200 za nishati jadidifu 2025

Spread the love

 

KAMPUNI ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), imesema mipango yake, ifikapo mwaka 2025 iwe imezalisha megawati 200 za nishati jadidifu na megawati 500 za joto, ambazo zitaweza kuingia kwenye gridi ya taifa, kukuza uchumi na kutunza mazingira. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Megawati hizo 200 ni katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ambapo marajio ifikapo 2025 kuwepo na megawati 1,100 za nishati jadidifu.

Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Kato Kabaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mchango wa kampuni hiyo, katika miaka 60 ya Uhuru Tanzania Bara.

Aliweka wazi uwezo wa jotoardhi kuzalisha umeme ni megawati 5,000 katika maeneo 50 ya mikoa 16 nchini.

Mhandisi Kabala aliitaja baadhi ya mikoa ambayo rasilimali jotoardhi inapatikana nchini ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera na mingine mingi.

Alisema jotoardhi ni umeme unaozalishwa kutumia shinikizo la mvuke pamoja na joto ambalo husukuma na kuzungusha mitambo ya kuzalisha umeme.

Mhandisi Kabaka alisema pamoja na Tanzania kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 5,000 za umeme wa jotoardhi pamoja na megawati 15,000 za joto kwa ajili ya matumizi ya kilimo, afya, ufugaji, viwanda na mengine.

“Tumeanza mchakato wa utafutaji megawati 200 za nishati jadidifu itokanayo na jotoardhi katika maeneo Ngozi Mbeya megawati 70 ambapo gharama zake ni takribani dola za Marekani milioni 144,” alisema.

Kabaka alisema utekelezaji wa mradi huo ikiwa pamoja na utafiti na uhakiki ulianza mwezi Septemba 2015 na unatarajiwa kukamilika ifikapo 2023 ambapo kwa sasa hatua iliyofika ni uchorongaji wa visima vya uhakiki.

Meneja huo alitaja mradi mwingine ni Songwe ulioanza 2018, ambao utazalisha megawati tano za umeme na matumizi mengine na utagharimu takribani dola milioni 32.

Alitaja mradi mwingine ni Kiejo Mbaka ulipopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ulioanza mwaka 2017, ambao unatarajiwa kutoa megawati 60 ambapo hatua za utafiti wa awali utaweza kuzalisha megawati 10 na utakamilika mwaka 2024 na utagharimu takribani dola za Marekani milioni 75.

Alisema kwa sasa mradi upo katika hatua za uhakiki rasilimali ya jotoardhi kwa kutumia visima vya uhakiki vitakavyochorongwa eneo la mradi.

“Hatua ya kwanza itakuwa ni uchorongaji wa visima vitatu cya utafiti kwa urefu wa mita 300/75 sentigredi kila kimoja ikiwa na lengo la kuongeza taarifa za kisayansi ambazo zitatoa tathmini bora ya kuchoronga visima virefu,” alisema.

Kabaka alisema hatua ya pili itakuwa kuchoronga visima vinne virefu vya mita 1,500 hadi 1,900 vya uhakiki na baada ya kukamilika hatua hiyo mradi utaingia katika hatua ya uendelezaji ikiwa ni pamoja na kuchoronga visima vya uzalishaji.

Mhadisi huyo alitaja miradi mingine ni Luhoi mkoani Pwani utakazalisha megawati tano, Natron mkoani Arusha megawati 60 ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2025.

Meneja huyo alisema miradi hiyo na mingine ikikamilika itaongeza mnyororo wa thamani katika maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi kama viwanda, kilimo, ufugaji, madini, afya, utalii, michezo, sayansi na teknolojia, maji safi na ajira.

Alisema katika utafutaji nishati ya jotoardhi pia yanapatikana madini, maji mvuke, maji moto, gesi na umeme jambo ambalo linasaidia sekta nyingine kuguswa hivyo mnyororo wa thamani kutokea.

Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila alisema serikali inavutia wawekezaji ili waje kuwekeza kwenye eneo la nishati jadidifu kwa kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Sisi kama Serikali tupo pamoja na TGDC, kuhakikisha kuwa rasilimali hii ya jotoardhi ambayo tumebarikiwa inawekezwa ili kutumika hasa kukabiliana na changamoto za umeme nchini. Tutaendelea kuwasiliana na wawekezaji mbalimbali nje na ndani ili waje wawekeze kwenye eneo hili,”alisema.

Mhandisi Rwebangila alisema dunia kwa sasa inahamia kwenye nishati jadidifu hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuungana na Serikali kwenye mpango huo uli uweze kufanmikiwa.

error: Content is protected !!