August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TFS kunufaisha wafugaji nyuki

Spread the love

KATIKA kuhakikisha wafugaji wa nyuki Kanda ya Kati wanafanya ufugaji wenye tija, Wakala wa Huduma za Mistu Kanda ya Kati (TFS) wameanzisha utoaji mizinga ya kisasa kwa wafugaji hao, anaandika Dany Tibason.

Akizungumza na mtandao huu Methew Kiondo, Meneja wa TFS Kanda ya Kati amesema, katika utoaji wa elimu, wameanzisha utoaji wa mizinga ya kisasa ambayo wafugaji hao wanakopeshwa kwa muda wa miaka mitano.

Kiondo amesema, mpango huo wa kuwakopesha mizinga wafugaji wa nyuki unaitwa kopa mzinga mmoja lipa chupa moja ya asali kwa mwaka.

Amesema, wakala wanawakopesha wafugaji wa nyuki mzinga ambao una thamani ya Sh. 75,000 ambapo mkulima atarejesha chupa moja ya asali kwa mwaka mmoja kwa kipindi cha miaka 5.

Kiondo amesema, chupa ya asaki ina thamani ya Sh. 10,000 hivyo kwa mwaka kipindi cha miaka mitano mfugaji huyo atakuwa kalipa kiasi cha Sh.50000 badala ya kulipa sh 75,000 ambayo ni thamani ya mzinga.

“Lengo la kuwakopesha mizinga ya kisasa ni kuwafanya kuwa na uwezo wa kuvuna asali bora na kwa kiwango kinachokubalika badala ya kutumia mizinga ya kienyeji.

“Hata ukiangalia kiasi wanachorejesha ni kidogo kwa maana bei ya mzinga ni Sh.75,000 lakini mfugaji anarejesha Sh 50,000 kwa kipindi cha miaka mitano na tunafanya hivyo kwa lengo la kujenga mahusiano kati ya mfugaji wa nyuki na TFS,” ameeleza Kiondo.

Amesema, juhudi hizo zinalenga kuwapatia elimu wafugaji wa nyuki ili kuweza kupata asali ambayo ni bora na yenye thamani huku wakiepuka kuua nyuki kwa kutumia zana ambazo si salama.

Amesema, kazi ya utoaji elimu kwa wafigaji wa nyuki ufanywa zaidi na maofisa ugani kwa lengo la kuwaelimisha wafugaji kupitia vikundi mbalimbali vya ufugaji nyuki.

error: Content is protected !!