January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TFDA yapiga ‘stop’ viwanda vinne

Spread the love

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imezuia viwanda vinne nchini kuendelea kutengeneza baadhi ya vipodozi vinavyosadikiwa kuwa na viambato vyenye sumu na vilivyopigwa marufuku. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hatua hiyo imekuja mara baada ya mamlaka hiyo kuendeleza mfumo wake wa ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa kwenye masoko ambapo walibaini uwepo wa baadhi ya vipodozi vyenye viambato vya sumu zinazozalishwa na viwanda hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo amesema kuwa, wamezuia uzalishwaji wa vipodozi katika viwanda vinne vilivyopo nchini sambamba na kingine kimoja kilichopo Afrika Kusini kusitisha uingizaji vipodozi hivyo kwa miezi sita kutokana na vipodozi hivyo kubainika kutokuwa salama.

Akitaja baadhi ya vipodozi ambavyo vimezuiwa kuzalishwa na viwanda hivyo, mkurugenzi huyo amesema kuwa ni pamoja na losheni, krimu na jeli ambavyo vinasadikiwa kuwa na viambato ambavyo vilipigwa marufuku kutokana na kuwa na aina ya steroids zinazojulikana kitaalam kama clobetasol propionate, hydrocortisone na triamcinolone.

“Tumeamua kuyazuia makampuni haya kutengeneza bidhaa za aina ya losheni, krimu na jeli kwasababu tulivyofinyanyia vipimo matokeo yake yalibainisha kuwa vipodozi hivyo vina viambato ambavyo si salama kwa binadam,” amesema.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, walibaini jumla ya vipodozi aina tofauti 36 vya jamii ya krimu na losheni kuwa na viambato vilivyopigwa marufuku baada ya kufanya uchunguzi wa kina wa matoleo 57 yaliyochukuliwa kwenye soko na viwanda vinavyotengeneza.

Akivitaja baadhi ya viwanda hivyo vilivyozuiwa kuzalisha vipodozi hivyo, kuwa ni, kiwanda cha Chemi and Cotex limited, Tridea Cosmetics Limeted vilivyopo jijini hapa, Mamujee Products Limited, Tanga Pharmaceutical and Plastics Limited vilivyopo Tanga, pamoja na kiwanda cha Johnson and Johnson (Pvt) Limited, Rattray Road, kilichopo Afrika kusini.

Amesema, sambamba na kuvizuia viwanda hivyo kutengeneza bidhaa hizo pia amewataka wenye viwanda hivyo kuviondoa vipodozi hivyo na kuviteketeza kwa gharama zao wenyewe.

“Mbali na hatua tulizochokua dhidi ya viwanda hivyo lakini pia tunakumbuka tuliwapatia usajili hivyo kutokana na hilo tunawafutia usajili hata kwa vipodozi vingine vilivyokuwa vimesajiliwa kutokana na kukiuka masharti ya mamlaka,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Dawa na bidhaa za niongeza, Adam Mitangu ametoa rai kwa wananchi kuacha kutumia vipodozi visivyokuwa na lebo husika sambamba na kuwataka wahusika wanaotengeneza vipodozi kuzingatia sheria ya chakula, dawa na vipodozi sura 219.

error: Content is protected !!