January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TFDA: Wananchi wanashiriki kuingiza bidhaa mbovu

Spread the love

UINGIZAJI bidhaa zisizo na ubora nchini unachangiwa na wananchi ambao hushiriki bega kwa bega na wafanyabiashara wasio waaminifu kukamilisha zoezi hilo, anaandika Regina Mkonde.

Gaudensia Simwanza, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma TFDA, amesema, mamlaka hiyo imeweka wakaguzi kwenye mipaka yote nchini ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa hizo lakini bado changamoto hiyo inaendelea kujitokeza.

“Mamlaka imehakikisha kila mpaka una wakaguzi ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi vigezo, lakini waingizaji hutumia njia za panya kuzipitisha bidhaa hizo,” amesema Simwanza na kuongeza;

“Baadhi ya wananchi hushirikiana na wahalifu kuingiza bidhaa hizo kinyemela, wengine huwaficha. Hili ni tatizo kubwa kwasababu linarudisha nyuma jitihada za TFDA za kumaliza tatizo hilo.”

Katika harakati za kukabiliana na tatizo hilo Simwanza amesema, Julai hadi Desemba mwaka jana TFDA imeteketeza bidhaa zenye thamani ya Sh. 798 milioni.

Simwanza ameueleza mtandao wa MwanaHALISI Online jijini, Dar es salaam leo kwamba bidhaa zilizoteketezwa zilikuwa si salama, bora na zimekwisha muda wake wa matumizi.

“Kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2015, mamlaka iliteketeza bidhaa zilizobainika kutokuwa na ubora na usalama kwa matumizi ya walaji zilizokamatwa nchi nzima, zilikuwa na thamani ya shilingi milioni 798,” amesema na kuongeza;

“Mamlaka itaendelea kudhibiti na kuteketeza chakula, vipodozi, dawa na vifaa tiba visivyo salama na ubora ili kulinda afya za watumiaji.”

error: Content is protected !!