TETEMEKO la ardhi lenye kipimo cha 6.4 limeua watu watatu jana tarehe 20 Februari 2023 na kujeruhi wengine zaidi ya 200 katika baadhi ya maeneo ya Uturuki yaliyoharibiwa wiki mbili zilizopita na tetemeko kubwa lililoua maelfu ya watu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Majengo zaidi yaliporomoka na kuwanasa baadhi ya watu, huku kukiripotiwa idadi ya watu wengi waliojeruhiwa katika nchi jirani ya Syria.
Kitovu cha tetemeko la Jumatatu kilikuwa katika mji wa Defne, katika mkoa wa Uturuki wa Hatay, eneo lililoathirika vibaya katika tetemeko la tarehe 6 Februari 2023 la kipimo cha 7.8.
Tetemeko la Jumatatu lilisikika pia nchini Syria, Jordan, Cyprus hata nchini Misri, likifuatiwa na tetemeko la pili la kipimo cha 5.8.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman Soylu amesema watu watatu waliuawa na 213 kujeruhiwa.
Juhudi za kuwatafuta na kuwaokoa manusura zilikuwa zikiendelea katika majengo matatu yaliyoporomoka ambako watu sita wanasadikiwa wamenaswa.
Leave a comment