Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko TEMESA wapewa mwezi mmoja kubadilika
Habari Mchanganyiko

TEMESA wapewa mwezi mmoja kubadilika

Spread the love

WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wamepewa mwezi mmoja kubadilisha utendaji kazi wao na kuleta matokeo chanya katika kutekeleza majukumu yao. Anaripoti Suleiman Msuya… (endelea).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi Aisha Amour ametoa rai hiyo jana alipotembelea Wakala huo kuongea na Watumishi pamoja na kukagua eneo la kivukoni na karakana ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam inayokifanyia ukarabati mkubwa kivuko cha MV. KAZI.

Balozi Aisha amewataka kusimamia nidhamu katika utendaji katika kitengo cha matengenezo ya magari kwani ndio iliyobeba taswira ya Wakala hivyo wahakikishe magari yanayotengenezwa yanakidhi thamani ya fedha ili kuepuka malalamiko ya wateja.

“Hakikisheni mnajipanga upya kwenye ukaguzi wa vivuko ili kuepusha kupeleka vivuko vikiwa kwenye uharibifu mkubwa na kwa upande wa magari hakikisheni mnatumia vipuri vyenye ubora unaotakiwa” amesema Balozi Aisha.

Amesema mwezi mmoja aliowapa wautumie katika kujipanga ili kuhakikisha gharama za kutengeneza magari zinapungua na kuendana na matengenezo wanayofanya na pia kuangalia upya Rasilimali Watu kama inakidhi mahitaji yao.

“Punguzeni kufanya kazi kwa mazoea na watumishi wanaoharibu taswira ya TEMESA wachukuliwe hatua’’, ameongeza Balozi Aisha.

Aidha, Balozi Aisha amewapongeza kwa hatua ya haraka waliyochukua kupeleka kivuko cha MV.KAZI kwenye matengenezo makubwa ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea endapo wangechelewa kukifanyia ukarabati huo mkubwa.

Ameongeza kuwa Serikali itatenga fedha za manunuzi ya kivuko kipya kitakachotoa huduma katika eneo la Magogoni na Kigamboni mkoani Dar es Salaam ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuboresha huduma eneo la Kigamboni.

“Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 500 sawa na abiria 2,000 na magari 60 na tayari fedha zimeshatengwa kwenye bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2022/23”, alisema Balozi Aisha.

Awali akitoa taarifa kwa katibu mkuu, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala alisema serikali imefanya maboresho ya ukataji tiketi kwa kusimika mfumo mpya wa kielekroniki (N-CARD) wa kusimamia mapato katika eneo hilo.

“Mfumo huo unaondoa mfumo wa zamani wa kutumia tiketi za karatasi na tayari tumeona mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa abiria katika sehemu ya kukatia tiketi,” alisema Kilahala.

Aliongeza kuwa abiria ambao wanatumia kivuko hicho kwa nadra wamewekewa utaratibu wa kadi za muda watakazozitumia wakati wa kuvuka katika eneo hilo.

Balozi Aisha alifanya ziara katika eneo hilo ili kukagua uendeshaji wa vivuko hivyo ikiwa ni pamoja na kuangalia masuala ya rasilimali watu, usalama wa watumiaji kivuko pamoja na kujadili namna bora ya kuboresha huduma katika eneo hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!