January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TEMCO: NEC imeandikisha 23,782,558

Spread the love

TAASISI ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO) imesema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeandikisha wapiga kura 23,782,558. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Hata hivyo taasisi hiyo imetoa taarifa ya awali ya timu yake ya uangalizi wa uchaguzi nchini kuhusu uandikishwaji wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa njia ya Kielektroniki (BVR).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Mwenyekiti wa TEMCO, Dk. Benson Bana amesema, taarifa hiyo iliandaliwa baada ya kuanza kwa zoezi la uadikishwa wa wapiga kura kati ya 23 Februari na 4 Agosti mwaka huu.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeandikisha jumla ya wapiga kura 23,782, 558 kati ya wapiga kura 23, 913, 184 waliotarajiwa ambao ni sawa na asilimia 99.6 ya lengo. Hii ni idadi kubwa sana ya wapiga kura na mafanikio kwa tume,” amesema Bana.

Bana amesema katika mchakato huo vyama vichache ndio viliweza kuweka mawakala katika vituo vya kuandikisha wapiga kura ambapo idadi ilitofautiana kwa viwango. Chama Cha Mapinduzi (CCM) asilimia 98. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) asilimia 94, Chama cha wananchi – CUF asilimia 36, NCCR – Mageuzi asilimia 12, ACT – Wazalendo asilimia 10, UDP, asilimia tatu na TLP asilimia mbili.

“Takwimu zote zinaonesha kuwa katika vituo 10, 432 vya uandikishwaji tulivyoangalia, vituo 8, 398 (asilimia 80.5%”) vilifunguliwa ndani ya muda uliopangwa. Vituo 2,034 (asilimia 19.5) vilifunguliwa baada ya saa 2 asubuhi. Asilimia 64 ya vituo vilifugwa kwa wakati Asilimia 36 ya vituo vilifugwa baada ya saa 12 jioni,” amesema Bana.

Aidha, Bana amesema changamoto kubwa ambayo iliyoikabili NEC katika zoezi hilo ni uchache wa vifaa vya BVR ambapo tume ilihitaji vifaa 15,000 lakini ikapatiwa vifaa 8,000, ucheleweshwaji wa fedha za kugharamia shughuli hiyo na kutokuwepo na mfumo wa kuhakiki uraia wa walioandikishwa.

Hivyo, Bana ameitaka serikali kuwa na Katiba na sheria zinazohusu watu wake wote kuweza kupiga kura, hasa ambao wapo nje ya nchi, kuhakikisha inatoa elimu ya watu wazima ili wajue kusoma na kuandika, kuwe na mpango wa elimu ya uraia, NEC iwe na maafisa ngazi ya kata na wilaya ili kuandikisha wapiga kura muda wote na kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanaandikishwa kabla ya muda wa kupiga kura.

Taarifa hiyo ilihusisha halmashauri 140, kata 1, 216, vituo vya kupiga kura 9, 728 Tanzania Bara na wilaya 11, Shehia 88 na vituo 704 kwa upande wa Zanzibar.

error: Content is protected !!