July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Tembo Warriors watua kishujaa bungeni, Spika awapa neno

Spread the love

 

KWA mara ya pili, leo tarehe 16 Juni, 2022 Bunge limetengua kanuni ya 160 (1) ambayo inatoa masharti kwa wageni wasio wabunge kuingia ndani ya ukumbi na kuiwezesha Timu ya Taifa ya Soka la Walemavu (Tembo Warriors) kuingia mjengoni na kukalia viti vya wabunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mara ya kwanza Timu ya Taifa wasichana ya chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ iliingia ndani ya ukumbi wa bunge tarehe 7 Juni mwaka huu baada ya kutinga kuingia faina ya mashindani ya kombe la dunia nchini India.

Aidha, leo Tembo Warriors nao wamealikwa bungeni na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, mahsusi kwa ajili ya kupongezwa pamoja na kusalimiana ana kwa ana na wabunge na viongozi mbalimbali wa serikali kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya pongezi bungeni, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa amesema Tembo Warriors imeitoa kimasomaso Tanzania baada ya kufuzu kwenda kucheza kombe la dunia nchini Uturuki katika mashindano yatakayofanyika Oktoba mwaka 2022.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya Tembo Warriors kulishangaza Taifa kwa kuliwakilisha vema kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wenye Ulemavu wa viuongo (CANAF) kwa kufuzu kwenda kucheza kombe hilo la dunia nchini Uturuki.

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo yaliyoshirikisha zaidi ya nchi 13 Afrika na kufanyika jijini Dar es Salaam Tanzania huku Ghana wakitwaa ubingwa.

“Itakumbukwa juhudi za ushindi huo zilichagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyemuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenda kambini kuwaongeza ari na hamasa kwa wachezaji pamoja na kutoa kiasi cha Sh milioni 150 zilizosaidia kuituza timu ya Taifa pamoja na maandalizi mengine.

“Hakika ilikuwa wakati wa jasho damu, kufa au kupona kwa ajili ya kupambania masilahi ya Taifa,” amesema.

Amesema ili kupata nafasi hiyo Tembo Warriors walitoa mkong’oto wa bao 2-1 kwa timu ya Morocco, bao 1-0 kwa Sierra Leon 1-0 na bao 5-0 kwa Cameroon.

“Timu hii kwa sasa ipo kambini tangu mwezi Februari 2022 kwa ajili ya maandalizi ya kombe la duniani yatakayofanyika nchini Uturuki kwa mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.

“Serikali ndio inagharamia kambi hiyo kwa matumizi yote ikiwamo, malazi, chakula, ufundi, usafiri wa ndani nan je pamoja na poisho za wachezaji na benchi la ufundi,” amesema.

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa

Amesema katika kuboresha maandalizi ya timu hiyo tarehe 9 hadi 13 Juni mwaka huu, timu hii ilishiriki michezo mitatu ya kimataifa ya majaribio nchini ambayo ilijumuisha nchi ya Morocco, Italia, Uingereza na Poland.

Amesema timu hiyo ilishinda mechi moja katika mashindano hayo pamoja na kwamba haikuchukua ubingwa lakini mchezaji wa Tembo Warriors, Alphan Athuman Kianga aliibuka mchezaji bora kwa kuweka kapuni magoli sita.

“Ndiye alikuwa mfungaji bora na kutunukiwa tuzo ya mfungaji bora, pia ilipewa tuzo ya kuwa timu bora na yenye nidhamu katika michuano hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa kambi ya timu hiyo sasa inahamia Karatu mkoani Manyara mahali penye utulivu zaidi na ukimya ili wamalizie maandalizi yao kabla ya kwenda Uturuki.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau ikiwemo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itahakikisha timu hiyo inaendelea kupatiwa malezi na matunzo yanayostahili ili kufanya vizuri katika mashindano ya dunia yanayotarajiwa kuanza tarehe 28 Septemba hadi 9 Oktoba , 2022 nchini Uturuki,” amesema.

Tanzania itaungana na nchi nyingine kutoka Bara la Afrika ikiwemo Morocco, Misri Angola.

Amesema mkakati wa wizara ni kwenda kubadilisha fikra za watanzania ya kuwa michezo ni sehemu ya burudani pekee la hasha! Duniani kote michezo ni ajira, ni biashara, ni utajiri.

“Kupitia program yetu ya mtaa kwa mtaa tunakwenda kusaka na kuibua vipaji vya wanamichezo watakaokwenda kucheza michuano ya kulipwa huko duniani hususani soka la kulipwa huko Ulaya, majira zetu wengi wameshatoa wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa ulaya. Nasi tunakwenda huko,” amesema.

Aidha, Nahodha wa Tembo Warriors, Juma Kidevu akitoa salamu za timu kwa wabunge ndani ya Bunge hilo, amesema ushindi walioupata CANAF ulitokana na chachu ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaijali sekta ya michezo.

“Tunakwenda kuupiga tena mwingi na kuitangaza Royal Tour,” amesema.

Aidha Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson mbali na kuipongeza timu hiyo kwa niaba ya Watanzania amesema heshima waliyopewa na Bunge ni ya nchi nzima.

Amesema Watanzania wanawatazama na kuwategemea kwamba walivyofanya vizuri ngazi hii watafanya vizuri zaidi ngazi inayofuata.

“Na kuingia kwenu hapa ni ahadi kuwa Kombe mtarudi nalo kwa hiyo tunawatakia kilala kheri katka michezo iliyo mbele yenu.

“Kama mnavyofahamu nchi nzima inasema Rais Samia anaupiga mwingi na sisi wabunge tunajua Rais anaupiga mwingi, sasa muende na nyie huko kwenye kombe la dunia mkawaoneshe Tanzania kuna Rais anayeupiga mwingi,”amesema Spika Tulia.

error: Content is protected !!