May 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

TEHAMA kurahisisha kazi serikalini

Spread the love

 

WASIMAMIZI wa miradi mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) serikalini wametakiwa kutumia weledi wao kwa ajili ya kurahisisha miradi hiyo na shughuli mbalimbali za serikali, anaandika Dany Tibason.

Suzan Mlawi Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameeleza hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa miradi mbalimbali ya Tehama Serikalini inayotekelezwa chini ya mradi wa miundombinu ya Mawasiliano (RCIP-Tanzania).

Baadhi ya mifumo ya serikali inayotumia TEHAMA ni pamoja na mfumo wa wakala wa usajili wa vizazi na vifo kupitia wakala wa RITA, mfumo wa taarifa za biashara kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, mfumo wa taarifa za kitabibu kupitia Hospitali ya taifa ya Muhimbili.

“Mifumo yote hii na mingine ukiwemo Mfumo wa Taarifa za Ununuzi kupitia PPRA na Bohari Kuu ya dawa nchini (MSD), Mradi wa kupitia idara ya kumbukumbu na nyaraka za taifa na mradi wa kupitia OR-MKUU na Wakala ua Serikali Mtandao (eGA),” alisema Mlawi.

Alisema kuwa mwelekeo wa serikali ni kulenga kutumia fursa zitokanazo na TEHAMA katika kuboresha utendaji kazi wa serikali katika taasisi zake na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi.

Naye Arnold Mathayo Mkurugenzi msaidizi Idara ya Tehama Ofisi ya Rais –Utumishi, amesema ni wakati sasa wa kila idara kuwa na mafunzo ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha ufanisi wa kazi.

Mafunzo hayo yanayotolewa kwa maofisa wasimamizi wa miradi 62, wakuu wa vitengo vya TEHAMA 15 na maofisa ugavi 50 kutoka kwenye taasisi mbalimbali za serikali, yatafanyika kwa siku 13 kwa watumishi wa kada mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya matumizi sahihi ya TEHAMA.

error: Content is protected !!