Spread the love

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameziomba Serikali barani Afrika kuziondolea tozo karatasi za kuchapisha magazeti. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Balile ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Mei, 2022  jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani.

Kwa mujibu wa Balile bei ya karatasi hizo katika soko la dunia imeongezeka kwa asilimia 250 kutoka Dola za kimarekani 450 kwa tani mwaka jana hadi kufikia dola 1,500 hivi sasa.

Balile amesema gharama za kuendesha magazeti “zimepanda kwa kiwango cha kutisha bei ya karatasi duniani imepanda kutoka wastani wa dola 450 kwa tani mwaka jana hadi dola 1,500 nilipoangalia leo asubuhi, hili ni saw ana ongezeko la asilimia 250.”

“Tunakuomba mheshimiwa rais na serikali zote Afrika katika bajeti zenu za mwaka huu kuondoa kodi ya ushuru wa forodha na VAT kwenye karatasi za kuchapisha magazeti kwani magazeti yanatumika kuelimisha jamii si vema kuyaacha yakafa kutokana na gharama za uzalishaji,” amesema.

Hata hivyo, Rais Samia amemuagiza Waziri Nape kuliangalia suala hilo. Mbali na hilo Balile aliziomba Serikali kote duniani kuwalinda maisha ya waandishi wa habari wanapokuwa kazini.

“Waandishi wanaumiza waandishi na kupoteza maisha na bado watenda maovu asilimia 80 hawachukuliwi hatua ipasavyo au hawaguswi.

“Katika kuadhimisha siku hiyo tunaona umuhimu wa pande mbili Serikali na wanahabari kukaa pamoja na kutafuta mwafaka na namna ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi,” amesema.

Ametaja matukio yanayoziangusha nchi nyingi ikiwemo Tanzania ni pamoja na waandishi kupigwa, magazeti kufungiwa, kupigwa faini za kiholela, mitandao ya kijamii kufungiwa, kesi zinazotokana na uchapishaji kufunguliwa kama jinai badala ya madai na watu kufunguliwa mashtaka kwa kutoa maoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *