Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari TEF yawasilisha serikalini maboresho sheria za habari
HabariTangulizi

TEF yawasilisha serikalini maboresho sheria za habari

Spread the love

 

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limekabidhi serikalini mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazogusa tasnia ya habari nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TEF, Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deodatus Balile amekabidhi mapendekezo hayo leo Jumanne, tarehe 16 Novemba 2021, mjini Dodoma kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balile amesema muhtasari wa mapendekezo hayo uliowasilishwa unalenga kuiwezesha Serikali kuzingatia maoni ya wadau wa habari, katika mchakato wa marekebisho ya sheria husika, kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa.

Balile amesema, mapendekezo hayo yanagusa sheria au baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo vinalalamikiwa na wadau wa habari nchini, kuwa vinakwaza uandishi wa habari pamoja na vyombo vya habari, katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Sheria zilizochambuliwa katika muunganisho huu ni Sheria ya Huduma za Habari ya 2016, Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa 2016 na ile ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) Kanuni, 2020 na Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, 2015,” amesema Balile.

Balile ametaja baadhi ya mambo ambayo wadau wa tasnia ya habari wanaomba kufanyiwa marekebisho au kubadilishwa kwa Sheria hizo, ni mamlaka ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), ambayo inaweza kufungia vyombo vya habari vinapodhaniwa au kutuhumiwa kuwa vimekosea.

Bila suala au makosa husika, kufikishwa katika vyombo vya kisheria vya kiuamuzi kama Mahakama.

“Wadau tunaona kuwa kifungu kama hiki kinamnyima mtuhumiwa nafasi ya kujitetea na kinakiuka kanuni ya msingi ya chombo kusikilizwa kabla kuhukumiwa,” amesema Balile.

Mwenyekiti huyo wa TEF, ametaja suala jingine ni Sheria ya Huduma za Habari (MSA), kuanzisha vyombo vinne vya kusimamia sekta ya habari, tofauti na sekta au taaluma nyingine ambako masuala husika husimamiwa na chombo au mamlaka moja.

“MSA inaanzisha Accreditation Board (Bodi ya Ithibati), Mfuko wa kusomesha waandishi wa habari na Independent Media Council (Baraza Huru la Habari), sisi katika hili tunapendekeza kuwapo kwa chombo kimoja pekee cha kuratibu sekta badala ya kuwa na vyombo vingi,” amesema Balile.

Amesema mchakato mzima wa kupata maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa, umehusisha wadau wa habari kupitia Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CORI), unaounganisha taasisi 11 chini ya Uenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Pamoja na TEF, wadau wengine waliotoa mapendekezo yao ni Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA – TAN) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Wengine; ni Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (CIB), Twaweza, SIKIKA na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Amesema katika mchakato huo pia, kulikuwa na fursa ya kupata maoni ya wahariri na baadhi ya wawakilishi wa Vilabu vya Waandishi wa Habari vya mikoa (Regional Press Clubs), katika kusanyiko lililoitishwa na TLS mjini Dodoma.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Kijaji amesema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo hayo, ili kuiwezesha sekta ya habari kuwa rafiki kwa wadau wake, hususan waandishi wa habari.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha sekta ya habari inakuwa rafiki na ni dhamira yetu sote kupiga hatua na kufikia malengo ya ufanisi utakaokuwa na faida kwa kila mmoja. Hatua ya leo ni mwanzo mzuri na ninaamini tutapiga hatua kwa faida ya taifa letu,” amesema Dk. Kijaji.

Baada ya kupokea mapendekezo hayo, waziri huyo ameyakabidhi kwa Katibu Mkuu wake, Dk. Zainab Chaula pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Jim Yonazi kwa ajili ya kuanza kuyafanyiwa kazi.

“Kazi ndiyo imeanza, hakuna kusubiri, kwahiyo baada ya kuyapokea naomba na mimi nikukabidhi Katibu Mkuu kwa ajili ya kuyafanyia kazi,” amesema Dk. Kijaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia atua Uturuki kwa ziara ya siku 5

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumatano amewasili nchini Uturuki kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda kung’oka tena

Spread the loveUWEZEKANO wa Paul Makonda, kuendelea na wadhifa wake wa mkuu...

error: Content is protected !!