July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TEF yamuonya Manara, kuisusia Simba

Haji Manara

Spread the love

 

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), wameutaka uongozi wa Klabu ya Simba umwonye, msemaji wake, Haji Manara kwa udhalilishaji alioufanya dhidi ya Mwandishi wa Habari wa Radio Clouds FM, Prisca Kishamba. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

TEF imesema, ikiwa vitendo vya aina hii vitaendelea kujitokeza, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari na vyombo vya habari, “hatutakuwa na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua zaidi Ili kuwaepusha wandishi wetu dhidi ya unyanyaswaji na udhalilishwaji.”

Jukwaa hilo, limetoa msimamo huo leo Ijumaa, tarehe 2 Julai 2021 na kusainiwa na mwenyekiti wake, Deodatus Balile, baada ya Manara kumdhalilisha Prisca, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.

Manara alikutana na waandishi wa habari tarehe 30 Juni 2021, jijini Dar es Salaam, kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga, utakaochezwa kesho Jumamosi, kuanzia saa 11: 00 jioni, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Taarifa yote ya TEF hii hapa;

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesikitishwa na linalaani kitendo cha Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara kumdhalilisha Mwandishi wa Habari wa Radio Clouds FM, Prisca Kishamba.

Udhalilishaji huo ulioambatana na maneno ya kashfa dhidi ya Prisca, ulifanywa na Msemaji huyo wa Simba kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Juni 30, 2021, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine, ulizungumzia mchezo wa Ligi Kuu ya Bara baina ya timu ambazo ni watani wa jadi; Simba na Yanga.

Kauli za vitisho vya Manara ni mwendelezo wa tabia na mwenendo wake dhidi ya Waandishi wa Habari ambao wamekuwa wakiripoti habari za Klabu ya Simba kwa maslahi mapana ya umma na Sekta ya michezo kwa ujumla.

Tukio la Juni 30 dhidi ya Prisca na Waandishi wa Habari wengine walipokuwa wakiuliza maswali kwenye mkutano huo, linafikirisha na linatufanya tutafakari ikiwa ni sahihi kwa vyombo vya habari kuendelea kuripoti habari zinazitolewa na Klabu ya Simba kupitia kwa Msemaji wake huyo.

Kimsingi vitendo vya aina hii vinavyofanywa na Haji Manara kwa Waandishi wa Habari siyo vya kiungwana na havivumiliki hata kidogo.

Wakati waandishi wa habari wanapokuwa kazini mara zote tumekuwa tukiwahimiza kufuata maadili ya kazi zao, vivyo hivyo kwa watoa habari wanapaswa kuwa waungwana hata pale wasipotaka kuyasikia maswali wasiyoyapenda.

Kwa tamko hili, tunamtaka Manara aache mara moja tabia ya kutumia mikutano ya Klabu ya Simba kwa Waandishi wa Habari na hata mitandao ya kijamii kuwadhalilisha wanahabari.

Ikiwa kuna suala lolote ambalo Mwandishi wa Habari amelitenda kinyume cha maadili na miongozo ya Taaluma ya Habari, wahusika wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwa taasisi za kihabari au kwa mwajiri wa Mwandishi husika Ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Kupitia taarifa hii pia tunaomba Uongozi wa Klabu ya Simba umwonye, Manara aache tabia hizi mara moja ambazo tunaamini hazina Afya na haziongezi thamani yoyote kwa Simba wala taaluma yetu ya Habari. Badala yake zinajenga chuki, uhasama na kuleta sintofahamu kwa pande husika.

Ikiwa vitendo vya aina hii vitaendelea kujitokeza, TEF kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari na vyombo vya habari hatutakuwa na njia nyingine zaidi ya kuchukua hatua zaidi Ili kuwaepusha wandishi wetu dhidi ya unyanyaswaji na udhalilishwaji.

Michezo ni furaha na siyo sehemu ya kujenga uhasama na uadui.

IMETOLEWA NA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)

DEODATUS BALILE
MWENYEKITI

DAR ES SALAAM, JULAI 02, 2021

error: Content is protected !!