Wednesday , 21 February 2024
Home Habari Mchanganyiko TEF watoa kauli nzito kwa Magufuli
Habari MchanganyikoTangulizi

TEF watoa kauli nzito kwa Magufuli

Spread the love

HOTUBA YA KAIMU MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF), DEODATUS BALILE KATIKA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI (WPFD) ILIYOADHIMISHWA KITAIFA MEI 3, 2018 JIJINI DODOMA, TANZANIA

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Mhe. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe

Ndugu Mwenyekiti wa MISA-Tanzania, Salome Kitomari,
Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kati Tanzania,

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi,

Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya,

Mwakilishi wa UNESCO, Anna Therese Ndong Jatta,

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Fausta Musokwa,

Mkurugenzi Mkazi wa Friendrich-Ebert-Stiftung (FES), Andreas Quasten,
Rais wa UTPC, Deo Nsokolo
Mkurugenzi Mtendaji Tamwa, Edda Sanga

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga
Waandishi Wakongwe (wazee wetu tulionao hapa),

Waandishi wa Habari wote,

Mabibi na Mabwana

Mheshimiwa Rais, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai sote tulioko hapa, na ni kwa neema zake kuwa leo tuko hapa kufanya shughuli hii muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya dola na vyombo vya habari kwa masilahi mapana ya maendeleo ya taifa letu.

Nakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu, kwani kwa kufanya hivi  Mhe. Rais umedhihirisha kwa matendo kauli yako uliyoitoa Bukoba ulipozungumza na waandishi wa habari waliokuwapo katika ziara yako kuwa “unawapenda waandishi wa habari, unawajali  na unawathamini.”

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

Leo ni siku ya maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Wajibu wa Uongozi: Vyombo vya Habari, Haki na Utawala wa Sheria. Siku hii inaadhimishwa kidunia katika Jiji la Accra, nchini Ghana. Kwa Tanzania, kitaifa inaadhimishwa hapa katika Jiji jipya la Dodoma.

Naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza waandishi wa habari wote nchini wanaofanya kazi hii ngumu ya kukusanya, kuchakata na kuchapisha habari na taarifa kwa nia ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Hongereni sana kuifikia siku hii muhimu katika historia ya uandishi wa habari.

Kila Mei 3, waandishi wa habari duniani kote huadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari; Siku hii inaadhimishwa kwa nia ya kupitia kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari duniani, kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kutoa heshima kwa waandishi waliouawa wakiwa kazini.

Mwaka 1993, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) ulipitisha azimio la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kutokana na Mapendekezo ya Mkutano wa 26 wa UNESCO uliofanyika mwaka 1991. UNESCO ilitoa maazimio hayo, baada ya Waadishi wa Magazeti barani Afrika kuwa wamekutana jijini Windhoek, Namibia, mwaka 1991 na kutoa azimio hili.

Hali ya Uhuru wa Habari nchini Tanzania

Mheshimiwa Rais, kabla ya Siku hii ya leo, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) tumefanya mikutano miwili kujadili hali ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania. Aprili 4, 2018 tulikutana jijini Dar es Salaam ambapo tulikuwa na mjadala wa kina juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari na kisha tukatoa tamko la TEF. Kati ya Aprili 26 hadi 28, mwaka huu Wahariri tumekutana Morogoro, ambapo nako tumepitia tena hali ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.

Kwa ujumla wake, Mhe. Rais tumebaini kuwapo hali ya kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini kutokana na matukio machache tunayoyataja hapa chini kati ya mengi yaliyojitokeza ndani ya mwaka huu wa kihabari tunaoumaliza.

1.     Mhe. Rais, Mazingira ya kazi kwa Wanahabari yamekuwa magumu kutokana na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola kuwabughudhi na kufanya uonevu wa wazi dhidi yao wanapokuwa kazini (rejea matukio ya polisi kuwanyanyasa waandishi wa habari wa Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na hapa Dodoma tulipo). Waandishi wamekuwa wakinyang’anywa simu zao, kuwekwa chini ya ulinzi na kuachiwa bila kufikishwa mahakamani, hivyo kuwatia wasiwasi wa kudumu.

2.     Tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, aliyepotea Novemba 29, mwaka 2017 ambaye hadi leo hajulikani alipo limeongeza hofu kwa waandishi wa habari hasa wale wanaoripoti habari za uchunguzi.

3.     Vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa na mamlaka kama Idara ya Habari –Maelezo (kwa magazeti) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) (kwa vyombo vya kielektroniki) na wakati mwingine kupewa adhabu kubwa za kulipa faini ama kufungiwa kama ambavyo hivi karibuni vituo vya televisheni vya Star TV, ITV, Azam, EATV na Channel 10 vimepigwa faini ya Sh milioni 65 na kuwekwa chini ya uangalizi kwa kutangaza habari zilizotokana na press conference iliyoitishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kuvituhumu eti haviku-balance habari hiyo.

4.     Hivi TCRA wanapotuita waandishi na kutueleza mpangilio wa masafa au baadhi ya vituo kunyang’anywa masafa mbona huwa tunatangaza habari hizo na hatupigwi faini kwa kuto – balance kwa walionyanganywa masafa? Nchi yetu imefika huko kweli?

5.     Mhe. Rais kuna kundi au watu wanaoitwawasiojulikana, wameleta hofu kubwa miongoni mwa waandishi wa habari, kwa kiwango ambacho katika historia ya nchi hii tumeshuhudia mwandishi Ansbert Ngurumo akikimbilia nje ya nchi kwa maelezo kuwawatu wasiojulikana walikuwa mbioni kuhatarisha maisha yake.

6.     Tukio la kuzuia Bunge Live, ambalo lilianza rasmi mwaka 2016 limeendelea kuwapo na kuwakosesha wananchi haki ya kupata habari.

7.     Mhe. Rais, Waziri Mwenye dhamana na masuala ya habari, amekuwa akitumia vibaya kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari kinachompa mamlaka ya kuzuia maudhui, lakini yeye amekikitumia kwa nyakati tofauti kufungia magazeti kama Mawio, Mwanahalisi, Mseto, Tanzania Daima and Raia Mwema.

8.     Kifungu hiki cha 59 kinasema: “The Minister shall have powers to prohibit or otherwise sanction the publication of any content that jeopardizes national security or public safety. Mantiki na msisitizo wa kifungu hiki upo kwenye maudhui (content) na si gazeti lililochapisha.

9.     Mhe. Rais, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia kwa Waziri Mwenye dhamana na masuala ya habari imetunga kanuni za kudhibiti mitandao ya kijamii za mwaka 2018 ambazo kiuhalisia hazitekelezeki. Zinatoa majukumu na wajibu, ambavyo ni vya kikampuni kwa mtu ambaye anaanzisha blog kuwasiliana na ndugu na jamaa, jambo linalokiuka haki za msingi za binadamu.

10.   Yamekuwapo matukio ya watendaji wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuviandama vyombo vya habari vinavyofanya kazi ya kuonyesha kinachoendelea nyakati za uchaguzi (kwa mfano kuibwa na kurejeshwa kwa sanduku la kura pale Kinondoni), waandishi kuitwa na kuhojiwa bungeni na mengine mengi.

Mhe. Rais, hali inayoendelea nchini na baadhi ya matukio niliyoyataja, hayana afya kwa taifa letu huko tuendako.

Tunayo mifano ya nchi nyingi duniani,zikiwamo zile ambazo ni majirani zetu, ambazo ziliingia katika gharama kubwa ya watu wake kwa kudharau matukio madogo madogo kama ambayo yanatokea nchini mwetu hivi sasa.

Sisi waandishi wa habari, tukiwa wataalamu wa habari, tunaowatangulia wenzetu kuona kinachotokea kwa jicho la kiuchambuzi, narejea wito wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa uhuru wa habari nchini, ambao hatima yake ni amani na maridhiano ya kitaifa, kwa kushirikisha wadau wengine wa habari, kabla hayajatukuta makubwa yaliyowakuta wenzetu. Tujifunze kwa wenzetu kwamba vyombo vya dola vinaweza kufanya kazi yake vizuri vikiwa vinaungwa mkono na raia wa taifa husika, bila kuviburuza vyombo vya habari.

Mwisho, si kwa umuhimu Mhe. Rais, natambua na kupongeza juhudi za serikali za kusimamia misingi ya uwajibikaji, vita dhidi ya rushwa na ufisadi, usimamizi wa mapato ya serikali, matumizi endelevu ya rasilimali za umma (hasa sekta ya madini), ujenzi wa miundombinu kama vile reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge, uimarishaji wa shirika la ndege (ATCL), kuhamia makao makuu Dodoma, usimamizi wa Sera ya Viwanda na mengine kadha wa kadha, ambayo ni vyanzo vya habari tunazozichapisha.

Hata hivyo, tunasisitiza kuwa maendeleo haya yatakuwa na maana zaidi kwa kuwa na taifa ambalo wananchi wake wanaishi kwa amani halisi na kuaminiana, bila kuogopa watu wasiojulikana.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakazi kwa mawaziri walia majitaka kusambaa mitaani

Spread the loveWAKAZI zaidi ya 4,000 wa mitaa ya Eyasi, TPDC na...

Habari Mchanganyiko

Viumbepori, bahari hatarini kutoweka

Spread the loveKUKOSEKANA juhudi za pamoja za Serikali, wadau wa uhifadhi na...

BiasharaHabari Mchanganyiko

TPSF yataja mbinu ya kuibua vipaji vipya taaluma ya madini

Spread the loveMkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga...

Habari Mchanganyiko

Kampuni 500 kushiriki maonyesho ya TIMEXPO 2024

Spread the loveSHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini  ( CTI) kwa kushirikiana na...

error: Content is protected !!