August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TEF: Tumetoka shimoni kwa mazungumzo

Deudatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF)

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mafanikio yaliyofikiwa katika kung’oa tasnia ya habari kwenye ‘shimo,’ hayakuhusisha mapambano bali mazungumzo na serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mtangazaji wa Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM, Scholastica Mazula kwamba, TEF imekuwa ikifanya kazi kwa maelekezo ya serikali.

Akijibu swali hilo Balile amesema, njia ya mazungumzo na serikali imeleta mafanikio makubwa na ndio maana, machakato wa mabadiliko ya sheria upo kwenye hatua nzuri.

“Kuna watu wanadhani kwamba, njia ya mapambano ndio inayoweza kubadilisha mazingira yaliyopo, sisi TEF tumechukua njia ya mazungumzio, ndio maana tunefanikiwa,” amesema Balile.

Ametaja mafanikio yaliyotokana na mazungumzo kati ya TEF na serikali kuwa ni pamoja na kufanikiwa kushawishi tasnia ya habari kuhamishiwa katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ambapo sasa inaitwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolijia ya Habari. Awali tasnia ya habari ilikuwa imeunganishwa na Michezo na Utamaduni.

Ameeleza kuwa, kanuni za ada kwa wamiliki wa televisheni walipaswa kulipa ada ya Tsh. 70 Mil lakini TEF na wadau wamefanikisha kuzungumza na serikali na kisha kushusha ada hiyo na kuwa Tsh. 30 Mil.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kurejeshwa kwa channel za televisheni za bure kwenye ving’amuzi vyote ambapo awali zilipelekwa kwenye vifurushi vya kulipia.

Ametaja mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari, ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya TEF ya sasa.

“Yote haya sidhani kama yanalenga maslahi binafsi, ukumbuke haya tumeyafanya ndani yam waka mmoja, hivyo nadhani mtu anayesema kuwa TEF ya sasa imejielekeza kwenye maslahi binafsi, afikiri upya kauli yake,” amesema.

Akizungumzia mabadiliko ya sheria za habari amesema, sheria ikitungwa ili kudhibiti habari, huwa na matatizo yaliyojificha, lakini ikiwa ni wezeshi, hutoa fursa ya kupata mawazo mapya yanayolenga ufanisi zaidi.

“Unapotunga sheria ya kuzuia ama kuminya habari, ujue kuna madhara makuba unayatengeneza hapo mbele. Ndio maana tunazungumza na serikali ili tuwe na sheria zinazokubalika kimataifa.

“Tusifurahie kutunga sheria mbaya kwa ajili ya kuumuza wengine, tusitunge sheria kwa ajili ya kukomoa waandishi bali tutafute ufanisi katika tasnia ya habari,” amesema.

error: Content is protected !!