JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kutofurahishwa na hatua ya Job Ndugai, Spika wa Bunge kuzuia waandishi wa habari kuzungumza na wabunge baada ya kuamua kutoka nje ya ukumbi wa bunge. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Leo tarehe 4 Aprili mwaka 2019, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadhi kutoka Chama cha Wananchi (CUF) waliotoka nje wakionesha kukasirishwa na hatua ya Bunge kumwadhibu Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini kutohudhuria Mikutano mitatu ya Bunge.
Baada ya wabunge hao kutoka nje, Spika Ndugai aliagiza kuwa, wasizungumze na waandishi wa habari na kuonya kwamba, atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua.
Adhabu hiyo ilitolewa leo baada ya Lema kuitwa kwenye kikao na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge jana kueleza sababu za kuunga mkono kauli ya Halima Mdee, Mbunge wa Kawa kwamba, Bunge ni dhaifu.
Mdee alitoa kauli hiyo akiunga mkono kauli ya Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyoitoa mwaka jana akiwa Marekani kwamba, Bunge ni dhaifu.
Deudatus Balile, Kaimu Mwenyekiti wa TEF amesema kuwa, Spika Ndugai amepotoka kwa kauli hiyo kutokana na kusigina ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri inayoeleza uhuru wa kujieleza na kutoa habari.
Balile amesema, “spika kazungumza hayo labda kwa sababu ya joto lakini amekosea.”
Amesema kuwa, kifungu cha saba na kifungu kidogo cha kwanza kinatambua haki ya mwanahabari hivyo, Spika Ndugai amekiuka sheria aliyoshiriki kuipitisha mwenyewe.
Leave a comment